Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu.
Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu hapa nchini inatarajia kuwafikisha Mahakamani wadaiwa sugu ambapo hadi sasa kuna jumla ya wadaiwa sugu 142,470 wenye mikopo ya shilingi 239,353,750,170.27 iliyokwishaiva hawajajitokeza wala kuanza kulipa mikopo yao.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo AbdulRazaq Badru wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo amesema mbali na kutoa siku 30, bodi hiyo inakamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani kwa kuvunja sheria ya bodi ya mikopo kifungu cha 19A(1).
Badru amesema kuwa bado kuna wanufaika wengi waliokopeshwa, muda wa matarajio ukapita bila kuwasilisha taarifa zao na kulipa madeni ya mikopo waliyokopeshwa tangu mwaka wa masomo 1994/1995.
Hatua nyingine ni pamoja na kuyawasilisha majina hayo katika taasisi za mikopo, kuwasiliana na wadhamini wao pamoja na kuyatangaza hadharani majina ya wadaiwa sugu wote ili waajiri, wadhamini na wadau wengine wayajue na kutoa taarifa katika bodi hiyo.
Kuhusu takwimu za mikopo iliyotolewa, amesema tangu 1994/95 hadi 2015/16 jumla ya shilingi 2,595,932,575.56 zimekopeshwa kwa jumla ya wanufaika 379,179.
Amesema kati ya mikopo yote iliyokopeshwa, mikopo iliyoiva ni shilingi 1,425,708,285,046.48 kwa wanufaika 238,430 ambao tayari wamemaliza kipindi chao cha matazamio.
Badru amesema kuwa jumla ya wanufaika wa mikopo 93,500 wamebainika na kupelekewa ankara za madeni yao, ambapo kati yao wanufaika 81,055 wanaendelea kulipa.