Clinton alaumu FBI kwa kushindwa kwake
Aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais wa Marekani kwa tikiti ya Chama cha Democratic Hillary Clinton, amesema kwamba kushindwa kwake ghafla katika uchaguzi uliyopita, kulichangiwa pakubwa na hatua ya mkurugenzi wa shirika la kijesusi la Marekani FBI, James Comey kutangaza uchunguzi mpya wa sakata ya barua pepe dhidi yake muda mfupi kabla ya uchaguzi.
Bi Clinton amewaambia wafadhili wa chama chake kwamba hatua ya Comey ilisambaratisha kampeini yake, licha ya uchunguzi huo kutompata na hatia.
Mwandishi wa BBC nchini Marekani hata hivyo amesema wengi wanahisi kuna msururu wa sababu zilizomfanya Donald Trump kumshinda katika uchaguzi huo.
Maelfu ya waandamanaji walifanya maandamano kwa siku nne mfululizo dhidi ya rais mteule Donald Trump.
Mjini New York ,maafisa wa polisi waliwazuia waandamanaji waliojaribu kukaribia bustani ya Union Square.
Wengine walielekea katika jumba la Trump Tower,nyumbani kwa bwana Trump pamoja na makao makuu ya biashara za Trump.