Trump Alivyowaliza Wabunge Dodoma
Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson amesema wabunge wanawake wamesikitishwa na kushindwa kwa mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Democrat, Hillary Clinton.
Dkt. Tulia ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma jana, baada ya kutambulisha wageni mbalimbali.
Amesema walitarajia mambo yangekuwa mazuri upande wao akina mama (wanawake), lakini haikuwezekana.
“Safari hii haikuwezekana, asikate tamaa maana baada ya miaka minne mambo yanaweza kuwa mazuri zaidi kuliko ilivyokuwa sasa. Nampa pole mama Clinton kwa kuwa safari hii haikuwezakana,” amesema Dkt. Tulia huku akishangiliwa na wabunge wanawake na kuongeza:
“Nasikia kuna watu hapa wanasema tungempeleka mheshimiwa fulani… katika maeneo yale mama Clinton angeshinda,” amesema.
Kutokana na kile kilichoonekana kupigwa butwaa na uchaguzi huo, kabla ya kuuliza swali la nyongeza jana asubuhi, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema), alisema ana masikitiko makubwa kwa sababu Hillary Clinton ameshindwa uchaguzi.
“Kwa niaba ya wanawake wenzangu, nampa pole mama Clinton kwa kushindwa uchaguzi, tumeumia sana na tumerudi nyuma,” amesema.
Kauli hiyo ilimfanya Dk. Tulia kumtaka aeleze amepata wapi taarifa wakati bado wabunge wanawake wana faraja Hillary angeweza kushinda.
Hata hivyo, akijibu swali la Suzan, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Khamis Kigwangala, alimpa pole Hillary kwa kushindwa kwenye uchaguzi huo.