Monday, 14 November 2016

Madini Ya Bilioni 3 Yakamatwa Yakitoroshwa

madini

V 2

Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) umekamata madini yenye thamani ya Shilingi 3,353,421,381.4 yakitoroshwa katika viwanja vikubwa vya ndege na katika matukio 25 tofauti.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TMAA, Mhandisi Dominic Rwekaza ameeleza hayo katika ripoti ya ukaguzi iliyofanywa na wakala huo mwaka 2015 na kudai kuwa katika kufuatilia usafirishaji wa madini nje ya nchi katika viwanja vikubwa tulikamata madini yanayotoroshwa yenye thamani ya Dola za Marekani 1,512,186.61 na mengine ya Shilingi 34,670,794 katika matukio 25 tofauti.

Kuhusiana na suala la migodi mikubwa kuwa na viwanja vya ndege kwa ajili ya kusafirishia madini, wakal huo umesema kuwa suala hilo haliepukiki kwa sababu za kiusalama.

Akifafanua ripoti ya ukaguzi wa madini ya mwaka 2015, Msemaji wa TMAA, Isambe Shiwa alisema licha ya kudhibiti utoroshwaji huo viwanja vya ndege vinatumika kusafirishia madini kutoka migodini moja kwa moja kwa sababu za kiusalama.

“Katika maeneo yote ya madini, kuna mawakala wa ukaguzi wa madini, wanashuhudia uzalishaji wa madini, hasa kwa dhahabu wana chukua mikuo (mche wa dhahabu) yake na kuileta kwenye maabara zetu ili ipimwe kujua kiasi cha dhahabu na fedha kisha wanakokotoa mrabaha kulingana na madini husika,” alisema.

Haya yanajiri ikiwa ni siku chache baada ya Rais John Magufuli kusema kuna utoroshaji mkubwa wa madini kupitia viwanja vya ndege vilivyopo migodini.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini hivi karibuni jijini, Rais Magufuli alisema pamoja na kwamba Tanzania ina utajiri mkubwa wa madini, kumekuwa na utoroshwaji wa madini kwa ndege zinazoruka kutoka kwenye baadhi ya migodi.

“Tuna dhahabu ambazo zinachimbwa, lakini utakuta watu wanasafirisha makontena ya mchanga unapelekwa kwenda kusafishwa na sisi ndiyo tunasindikiza na wananchi mpo mnashangilia,” alisema Rais Magufuli.

“Kwa sababu kule wanakwenda ku­separate (kutenganisha). Kwa nini tusijenge separation plant hapa tukatengeneza ajira hapa kwa Watanzania,” alihoji.

clouds stream