Tarehe
November 6, 2015
Rais mstaafu wa awamu wa nne Dkt.Jakaya Kikwete.
Wafungwa 4,160 wamepata msamaha kutoka kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya
nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyekabidhi nchi kwa rais mpya Dkt.John
Pombe Magufuli aliyeapishwa jana jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mathias Chikawe kwa vyombo vya habari jana Dar es Salaam
imebainisha kuwa kati ya wafungwa hao, wafungwa 867 wataachiwa huru na
wafungwa 3,293 watapunguziwa vifungo vyao na kubaki gerezani wakitumikia
sehemu ya vifungo vyao vilivyobaki.
Amewataja walionufaika na msamaha huo kuwa ni wafungwa wote
wapunguziwe moja ya sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida
linalotolewa chini ya Kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya
58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika ibara ya 1 (i-xix).
Wafungwa wengine kuwa ni wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama
Ukimwi, kifua kikuu, saratani ambao wako kwenye hatua ya mwisho ambao
watathibitishwa na waganga chini ya Mganga mkuu wa mkoa au wilaya.
Ameongeza kuwa wazee wenye umri zaidi ya miaka 70, wafungwa wa kike
walioingia na mimba gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya na
wasionyonya na walemavu wa mwili na akili na ulemavu huo uthibitishwe na
jopo la waganga.
Katika hatua nyingine taarifa hiyo imesema kuwa msamaha hautawahusu
wafungwa wenye adhabu za kunyongwa, waliohukumiwa kunyongwa na adhabu
hiyo baadaye kubadilishwa kuwa kifungo cha maishaau kifungo gerezani.
Wengine ni wafungwa waliotumikia kifungo kwa makosa ya usafirishaji
na utumiaji wa dawa za kulevya, makosa yanayohusu uombaji, upokeaji na
utoaji rushwa, unyang’anyi na kujaribu kutenda makosa hayo, kubaka,
kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo.
Aidha, makosa mengine ambayo vifungo vyake haviko kwenye msamaha huo
ni makosa ya kuwapa mimba wanafunzi, wizi wa magari, pikipiki au
kujaribu kutenda makosa hayo, matumizi mabaya ya madaraka, waliowahi
kupunguziwa vifungo na Rais.
Wafungwa wengine ni wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi na
ubadhirifu wa fedha za Serikali, kutoroka au kujaribu kutoroka wakiwa
chini ya ulinzi halali na wafungwa wanaotumikia vifungo chini ya Sheria
ya Bodi ya Parole Sheria Namba 25 ya Mwaka 1994 ya Sheria ya Huduma kwa
Jamii Namba 6 ya Mwaka 2002.