Tarehe
June 15, 2015
Rais
Yoweri Museveni wa Uganda (kushoto) akiwa na aliyekuwa Waziri Mkuu na
Katibu Mkuu wa chama tawala cha NRM, Bw Amama Mbabazi. Bw Mbabazi
ametangaza kuwa atagombea kukiwakilisha NRM kwenye uchaguzi mkuu ingawa
chama hicho kilishatangaza rasmi kuwa Museveni ndiye mgombea pekee na
atakiwakilisha
Rais Yoweri Museveni amekuwa madarakani kwa karibu miaka 30 toka
alipotwaa madaraka mwaka 1986. Katika kipindi hiki chote amekumbana na
wapinzani wa aina tofauti tafouti.Amekumbana na wapinzani wa kijeshi
(waasi), amekumbana na upinzani ndani ya chama na serikali yake na wale
wa siasa wa vyama vya upinzani.
Mmoja wa wapinzani ambao amekumbana nao na ambao wameonekana
kumuhenyesha kweli ni yule aliyekuwa mtu wake wa karibu sana kiasi cha
kuwa daktari wake walipokuwa wakipagania madaraka, Kanali Mstaafu Kizza
Besigye.
Baada ya Museveni kutwaa madaraka, Besigye alikuwa mmoja wa kundi lililokuwa na madaraka katika jeshi na kwenye duru za Utawala.
Lakini mwaka 2001 Besigye alitangaza kumpinga Museveni upinzani ambao
hadi sasa pande zote, waganda na Ulimwengu unaukumbuka. Kwa mara mbili
mfululizo, mwaka 2006 na 2011 pande hizo mbili zilimenyana katika
uchaguzi mkuu, na mara zote Besigye akitangaza kuwa alikuwa ameshinda
isipokuwa Museveni aliiba kura.
Katika vinyanganyiro hivyo kulijitokeza sura ya serikali kutumia
nguvu sana kumdhibiti Besigye na wakati mmoja Besigye ‘alikimbilia’
uhamishoni nje ya Uganda akirudi baada ya muda. Besigye amekamatwa mara
kadha na kuswekwa ndani; moja ya operesheni za kumkamata zinazokumbukwa
mno ni ile yeye na abiria waliokuwa kwenye gari lake walipomwagiwa
pilipili kwenye gari yake na akaburuzwa hadi kwenye gari la wanausalama,
vitendo vilivopelekea akimbizwe hospitali Nairobi kwa matibabu.
Wapinzani na wapenzi wa Museveni wote wameongezeka toka mwaka 2001,
lakini hapajawepo mpinzani mwenye nguvu na ushawishi ndani ya chama
chake kama, Bw. Amama Mbabazi, mwanasiasa mkongwe na swaiba wa Museveni
kwa miaka mingi akishika nyadhifa tofauti Serikalini mara ya mwisho
akiwa Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wa Chama tawala cha Museveni cha NRM.
Amama Mbabazi akitangaza nia
Bw Mbabazi ni tofauti kwa sababu amejitokeza hadharani na kutangaza
kuwa atachuana na Museveni kukiwakilisha chama chao kama Mgombea wa
Urais, huku kamati ya chama hicho ikiwa tayari imeshatangaza kuwa
Museveni hatokuwa na mpinzani kwenye chama hicho.
Ni takribani miezi 8 sasa toka Mbabazi ayenguliwe kutoka kwenye
nyadhifa yake ya Waziri Mkuu, kuenguliwa kuliosemekana kutokana na
‘njama za wazi’ za kutaka na kujipanga kuwa Rais wa Uganda.
Katika kipindi hicho chote, kumekuwepo na sauti za chini chini kuwa
Mbabazi angeligombea Urais lakini yeye mwenyewe alikuwa hajasema wazi
wazi. Lakini sasa kaweka bayana kuwa atachuana na Museveni kwanza ndani
ya chama, na akiibuka kidedea atagombea Urais wa nchi ya Uganda.
Makamanda wawili wameshavaa magwanda, maswali matano muhimu ni je,
1. nani ataibuka kidedea?
2.Nini hatma ya atakayepoteza katika hawa wawili?
3. Nini hatma ya chama cha NRM?
4. Museveni, anayesifika kwa mbinu za kisiasa na vita, ataweza kuvuka kwenye uchaguzi 2016?
5. Je baada ya miaka 30 ya Museveni, Uganda imekomaa kiusalama, kidomkrasia na utawala kuweza kuhimili mitikisiko ya sasa?