Wednesday, 28 October 2015

UKAWA wapinga matokeo ya urais ya NEC


UKAWA wapinga matokeo ya urais ya NEC

Tarehe October 28, 2015
Mgombea urais wa Ukawa Edward Lowassa.
Vyama vinavyounda Ukawa, wamekutana kujadili mwenendo waliouita usio halali wa kutangaza matokeo, wakiituhumu Tume ya Uchaguzi (NEC), CCM na Jeshi la Polisi kushirikiana kuhujumu matokeo.
Kwa mujibu wa viongozi hao  ambao ni  Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, James Mbatia (mwenyekiti, NCCR Mageuzi) na Profesa Abdallah Safari, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wakizungumza  na waandishi wa habari jana Makumbusho jijini Dar es Salaam  wamesema  hawayatambui  matokeo  hayo  kwa  kuwa  yamechakachuliwa.
Mbowe alibainisha  kuwa kuna vijana kutoka Kenya, ambao wamewekwa hoteli mmoja Dar es Salaam ambao wanafanya kazi ya kuchakachua matokeo yanayotoka majimboni na baadaye kuyapeleka NEC.
Ameyataja  baadhi ya majimbo hayo kuwa ni Nyamagana, Rungwe, Kahama Mjini, Shinyanga Mjini, Kyela na Muleba Kusini.
“Kazi hii ya uchakachuaji matokeo inafanywa na CCM, inaratibiwa na NEC na wasimamizi wakubwa ni polisi,” alisema Mbowe.
Naye Profesa Safari alitoa mfano wa Jimbo laTandahimba ambako alisema NEC ilitangaza kuwa mgombea wa CCM, Dk John Magufuli alipata kura 49,098 na Lowassa kura 46,288 ambazo ni tofauti ya kura 280.
Lakini matokeo halisi kutoka kwa mawakala wetu yanaonyesha Lowasa alipata kura 44,537 na Dk Magufuli 44,253 ambazo ni tofauti ya kura 284,” alisema Profesa Safari.
Aliongeza kuwa  NEC ilitangaza kuwa Lowassa alipata kura 6,000 Jimbo laTunduma, wakati matokeo yao yanaonyesha alipata kura 32,442.
Akizungumzia  vijana waliokamatwa  Mbowe 191  ambao nane kati yao walifikishwa mahakamani jana kujibu mashtaka ya kufanya makosa ya kimtandao alisema kitendo hicho cha kuwanyima dhama hakistahili. Alisema kitendo cha polisi kuwakamata vijana hao waliokuwa wakijumlisha matokeo, kimevuruga mfumo wa ukusanyaji matokeo wa Chadema.
“Lakini sasa tunatumia fomu za mawakala wetu ambazo zinaonyesha (mgombea urais wa Chadema, Edward) Lowassa anaongoza kwa tofauti kubwa ya kura,” alisema Mbowe.
Alisema vijana hao wamekamatwa kwa kosa ambalo linafanywa na mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba ambaye Mbowe alisema amekuwa anatangaza matokeo ya uchaguzi na idadi ya majimbo bila ya kuchukuliwa hatua zozote.
Alipoulizwa kuhusu  utangazaji matokeo Makamba alisema kuwa hakuna tatizo la yeye kusema kuwa watashinda kwa asilimia fulani kwa sababu kila chama kimekuwa kikisema hivyo.
Mwenyekiti Mwenza Ukawa James Mbatia alisema “Hili ni janga la Taifa linalotengenezwa na binadamu huku wakijua athari zake.
Alisema kinachotokea ni kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kukataa mapendekezo ya vyama vya upinzani waliomtaka abadili mambo manne kwenye katiba kabla ya uchaguzi ambayo ni pamoja na matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani, kuruhusiwa kwa mgombea binafsi, mgombea urais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50 na tume ya uchaguzi kuwa huru.

Prof. Jay, Sugu, Baba Levo wapeta uchaguzi mkuu

Prof. Jay, Sugu, Baba Levo wapeta uchaguzi mkuu

Tarehe October 28, 2015
Msanii wa Hip hop, Joseph Haule ‘Prof. Jay’
Mwanamuziki mkongwe nchini Tanzania, Joseph Haule ‘Prof. Jay’, amechaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Mikumi mkoani Morogoro, kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo ‘CHADEMA’.
Prof. Jay, ambaye alikuwa anawania ubunge ametangazwa rasmi kuwa mbunge mteule wa jimbo hilo baada ya kupata kura 32,259 dhidi ya mpinzani wa karibu, Jonas Nkya wa CCM aliyepata kura 30,425.
Kupitia mtandao wa kijamii mwanamuziki huyo ameweza kubainisha kura alizopata na kudai kuwa amepata ushindi huo kwa tofauti ya kura 1834 na kuzidi kuwashuru wananchi wa jimbo hilo na Mwenyezi Mungu kwa ushindi huo.
Sambamba na hilo Mbunge wa Mbeya mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo ‘CHADEMA’, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ aliyekuwa mbunge jimbo hilo amefanikiwa kutetea jimbo lake kwa kupata kura zaidi ya elfu 67.

Naye mwanamuziki Baba Levo, ameibuka kidedea baada ya kushinda kura za udiwani, Kigoma Mjini kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, na kuwashukuru waliompigia kura.
Ameongeza kuwa japo anakuwa Diwani wa Kigoma mjini kwa miaka mitano lakini muziki hatouacha na atajitahidi pia kusaidia vijana wenye vipaji Kigoma, ili waweze kutambulika kwa sanaa wanazofanya.
Baba Levo
Hata hivyo kwa upande wa msanii wa filamu na mchekeshaji nchini, Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’, ameshindwa kutamba baada ya kukosa ubunge wa jimbo la Kisarawe kupitia Chama cha CUF.
Kingwendu, ambaye kura zake hazikutimia amedai kuwa awali alikuwa anaongoza kwa kupata kura nyingi lakini baada ya kura kuhesabiwa zilionekana kuwa pungufu na hivyo Suleiman Jafo, kuibuka kuwa mshindi.
“Nimejaribu na nimethubutu kwa mara ya kwanza kugombea nafasi kubwa ya Ubunge, nimeenda vizuri tu na sitachoka na wala sitaacha, najipanga tena kwa mara nyingine najua nimekosea wapi na nitajipanga upya na nitaenda kusomea siasa zaidi,”.

Magufuli aongoza hadi sasa; Raisi kujulikana kabla ya Alhamisi

Magufuli aongoza hadi sasa; Raisi kujulikana kabla ya Alhamisi

Tarehe October 28, 2015
Mgombea urais kupitia tiketi ya ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Pombe Magufuli.
Ikiwa ni siku mbili baada ya kura za uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba kuanza kuhesabiwa, mgombea wa kiti cha Urais cha Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt John Pombe Magufuli yuko mbele kwa matokeo yaliyo tangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguza (NEC).
Huku matokeo kutoka majimbo 113 kati ya ya jumla ya 264 yakiwa yamekwishatangazwa hadi Jumanne usiku, matokeo yanaonesha kuwa Magufuli ameshajizolea jumla ya kura 2,461,771 (aslimia 57.21) huku minzani wake wa karibu, Edward Lowassa akiwa amepata jumla ya kura 1,764,785 (asilimia 41.01).
Wagombea wa vyama vingine vya upinzani wamejizolea chini ya asilimia 2 ya kura hadi sasa hivi.
Akizungumzia mwenendo wa utangazaji wa matokeo ya kura hizo za Urais, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alifafanua kuwa matokeo mengine yatatangazwa kadri yatakavyopatikana na anategemea kuwa kati ya siku ya Jumatano na Alhamisi matokeo yote yatakuwa yamekwishakupatikana na Raisi mteule wa Jamuhuri ya Tanzania kwa miaka mitano ijayo kujulikana.

Tuesday, 27 October 2015

Ezekiel Wenje aangukia pua Nyamagana, adai demokrasia haijatendeka

Ezekiel Wenje aangukia pua Nyamagana, adai demokrasia haijatendeka

Tarehe October 27, 2015
Ezekiel Wenje akiongea na waandishi wa habari.
Mgombea wa Chama cha Mapinduzi ‘CCM’ Jimbo la
Nyamagana Mkoani Mwanza, ameibuka mshindi wa kiti cha Ubunge katika jimbo hilo na kumbwaga aliekuwa mbunge wa jimbo hilo Ezekiel Wenje, kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo ‘Chadema’.
Katika matokeo hayo Stanslaus Mabula ameibuka kidedea kwa kupata kura 81,017 na hivyo Ezekiel Wenje, kupata kura 79,280.
Matokeo hayo yalitangazwa na msimamizi mkuu wa uchaguzi jimboni Tito Mahinya, huku kukiwa na ulinzi mkali wa vyombo vya ulinzi na usalama katika viunga vya ofisi za Jiji hilo.
Akitakangaza matokeo hayo majira ya saa saba usiku wa kuamkia leo, Mahinya, alibainisha kuwa pia CCM imeibuka kidedea kwa upande wa Madiwani ambapo kati ya Kata 18, imeshinda Kata 14 na Chadema Kata nne.
Kwa upande wa Wagombea wengine, Chacha Okong’o (ACT Wazalendo) alipata kura 161, Faida Potea (CUF) amepata kura 1,005, Ahmad Mkangwa (NRA) kura 104, Mohamed Msanya (Jahazi Asilia) kura 175 na Ramadhan Mtoro (UDP) amepata kura 68. Hata hivyo kabla ya matokeo hayo kutangzwa, mgombea kutoka Chadema, Ezekiel Wenje, alikataa kusaini karatasi ya wagombea na kubainisha
kuwa demokrasia haikutumika katika zoezi zima la kuhesabu kura katika
uchaguzi huo na kwamba atafuata hatua zaidi za kisheria katika kupinga matokeo hayo.
Kwa upande wake Mshindi wa Uchaguzi huo Stanslaus Mabula, amesema kuwa tangu awali alitarajia ushindi huo na kwamba suala la demokrasia limezingatiwa.
Katika hatua nyingine Mabula, amedai kuwa atahakikisha anatatua changamoto zinazolikabili Jiji la Mwanza, ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha wakazi wa Jiji katika shughuli mbalimbali za uzalishaji ili waweze kujitegemea kiuchumi.

Picha: Mh. Joshua Nassari aibuka kidedea Arumeru Mashariki

Picha: Mh. Joshua Nassari aibuka kidedea Arumeru Mashariki

Tarehe October 27, 2015
Mbunge mteule wa jimbo la Arumeru Mashariki  Chadema, Mhe. Joshua Nassari akiwasalimia wafuasi wa chama chake
Mbunge mteule wa jimbo la Arumeru Mashariki kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mhe. Joshua Nassari ameibuka kidedea baada ya kupata ushindi wa kishindo kuwatumikia wananchi wa Arumeru Mashariki.

Utovu wa nidhamu waendelea kumwandama Mourinho

Utovu wa nidhamu waendelea kumwandama Mourinho

Tarehe October 27, 2015
Jose Mourinho
Jose Mourinho amefunguliwa mashtaka ya utovu wa nidhamu na Shirikisho la Soka la Uingereza kwa sababu ya lugha aliyoitumia na vitendo vyake wakati wa mechi ambayo Chelsea walichapwa na West Ham United wikendi.
Mourinho alifukuzwa eneo la marefa uwanjani baada yake kwenda kutaka kuzungumza na refa Jon Moss katika chumba chake wakati wa mapumziko mechi hiyo ya Jumamosi.
Klabu zote mbili pia zimeshtakiwa kwa kushindwa kudhibiti wachezaji na zimepewa hadi Oktoba 29 kujibu mashtaka hayo.
Chelsea tayari wanakabiliwa na faini ya £25,000 kwa wachezaji zaidi ya watano kupewa kadi za manjano wakati wa mechi hiyo ya Ligi ya Premia.
Kando na kadi mbili alizoonyeshwa Nemanja Matic, Chelsea pia walishuhudia wachezaji wao Cesar Azpilicueta, Willian, Cesc Fabregas, John Mikel Obi na Diego Costa wakilishwa kadi uwanjani Upton Park.


Msaidizi wa Mourinho Silvino Louro pia alifukuzwa eneo lake wakati wa mechi hiyo na vilevile ameshtakiwa kwa utovu wa nidhamu.
Klabu hiyo pia itatakiwa kueleza wasimamizi wa Ligi ya Premia ni kwa nini Mourinho alikosa kuzungumza na wanahabari baada ya mechi hiyo.
Mechi hiyo ilikuwa ya tano kwa Chelsea kushindwa katika mechi 10 za ligi msimu huu na inawaacha mabingwa hao watetezi wakiwa nambari 15 na alama 11, alama 11 nyuma ya viongozi Manchester City.

Matokeo ya Awali ya Uraisi Katika Majimbo ya Makunduchi, Paje na Lulindi

Matokeo ya Awali ya Uraisi Katika Majimbo ya Makunduchi, Paje na Lulindi

Tarehe October 26, 2015
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva ametangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais 2015 katika majimbo matatu kwa mujibu wa taarifa ya NEC ambapo majimbo hayo ni Makunduchi, Paje ya visiwani Zanzibar pamoja na jimbo la Lulindi -Mtwara.
Screen-Shot-2015-10-26-at-10.33.49-AM Screen-Shot-2015-10-26-at-10.34.00-AM Screen-Shot-2015-10-26-at-10.33.35-AM

CUF Kidedea Majimbo Manne Zanzibar


CUF Kidedea Majimbo Manne Zanzibar


Tarehe October 26, 2015
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jecha Salim Jecha akito taarifa kwa vyombo vya Habari kuhusiana na uchaguzi Mkuu.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeendelea kutangaza matokeo ya Ubunge pamoja na baraza la wawakilishi katika Majimbo manne ambayo ni  jimbo la Mtambile , Ngogoni, Mtambwe, Gando.
Kwa mujibu wa ZEC washindi wa Ubunge katika majimbo hayo ni kama Ifuatavyo:
Jimbo la Mtambile ni Masoud Abdallah Salim (CUF) ambapo ameshinda kwa Idadi ya kura 5,106, Mtambwe ni Khalifa Mohamed Issa (CUF) kwa  Idadi ya kura 5,663, Gando Othman Haji Omary (CUF) kwa idadi ya kura 6, 111 na Ngogoni ni Suleiman Ally Yusuf (CUF) kwa Idadi ya kura 5,660.
Wakati huohuo kwa upande wa Nafasi ya Baraza la Uwakilishi kutoka Mtambile Mshindi ni Abdalla Bakari Hassan kwa kura 5383.

Utata wagubika uchaguzi Jimbo la Kibamba

Utata wagubika uchaguzi Jimbo la Kibamba

Tarehe October 26, 2015
mnyika
Wakati maeneo mbalimbali ya nchi ya Tanzania yakianza kutangazwa kwa washindi wa Udiwani na Ubunge, hali ya sintofahamu imejitokeza katika baadhi ya kata na majimbo nchini.
Kata kadhaa zikiwemo maramba Mawili, Saranga na Mdezi Lius imeendelea, kutoeleweka na kupelekea kusababisha uchaguzi kurudiwa kwa baadhi ya sehemu hizo.
Lililojitokeza eneo la Kimara Stop Over ni pamoja kuchekewa kufika kwa vifaa vya uchaguzi na kutolipwa kwa kadiri ya makubaliano kwa mawakala.

Pamoja na hayo hali ni ya utulivu pamoja na kuwepo kwa wingi kwa wafuasi wa vyama na askari wengi katika maeneo mbalimbali. Mgombea ubunge kupitia tiketi ya CHEDEMA amekuwa akilalamika kuwa wanafanyiwa makusudi ya kuvuruga matokeo.
Mgombea ubunge kupitia tiketi ya CHEDEMA amekuwa akilalamika kuwa wanafanyiwa makusudi ya kuvuruga matokeo.

Maalim Seif Aitaka ZEC kutangaza Matokeo Halisi

Maalim Seif Aitaka ZEC kutangaza Matokeo Halisi

Tarehe October 26, 2015
Mgombea Uraisi wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Waandishi wa Habari.
Mgombea Uraisi wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Maalim Seif Sharif Hamad ameitaka tume ya Uchaguzi zanzibar kutangaza matokeo halisi kama ilivyo kwenye fomu zinazotoka vituoni.
Kwa mujibu wa Mgombea huyo akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi uliopita amesema kuwa baada ya chama chake kukusanya fomu zote za matokeo kutoka vituoni, matokeo yanaonyesha kuwa yeye amepata kura 200,007 dhidi ya kura 178,363 za mgombea wa CCM anayetetea nafasi yake Dokta Mohammed Shein, hivyo amehitaka tume ZEC kutangaza matokeo halali kulingana na takwimu zilizopo kwenye fomu.
Awali Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Salim Jecha, ametangaza matokeo ya uchaguzi wa urais wa Zanzibar kwa majimbo mawili ya Kiembesamaki na Fuoni, ambapo kwenye majimbo yote mawili mgombea wa CCM, Dokta Ali Mohammed Shein, anaongoza.
Zanzibar ilikuwa  na majimbo 54.

CCM yaongoza Zanzibar matokeo ya awali

CCM yaongoza Zanzibar matokeo ya awali

Tarehe October 26, 2015
matokeo
matokeo katika jimbo la Kiembe samaki.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Salim Jecha, ametangaza matokeo ya uchaguzi wa urais wa Zanzibar kwa majimbo mawili ya Kiembesamaki na Fuoni ikiwa ni motokeo ya awali.
Katika majimbo  hayo Mgombea urais wa CCM Dkt. AllI Mohammed Shein anaongoza.
Visiwani  Zanzibar  kuna   majimbo 54 yanayoshiriki uchaguzi mkuu uliofanyika jana  nchini kote. Katika hatua nyingine  Matokeo  ya  awali  Tanzania bara  yataanza  kutangazwa leo kuanzia  saa  4  asubuhi.

CCM yawataka wananchi ‘kuwalipua’ wavunjifu wa amani

CCM yawataka wananchi ‘kuwalipua’ wavunjifu wa amani

Tarehe October 25, 2015
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya CCM, Jakaya Kikwete akipiga makofi wakati alipowasili katika mkutano wa chama hicho hivi karibuni.
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya CCM, Jakaya Kikwete akipiga makofi wakati alipowasili katika mkutano wa chama hicho hivi karibuni.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wananchi katika meneo yote nchini kuripoti endapo kuna viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani katika kipindi cha upigaji kura na kutangazwa maotokeo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mjumbe wa Halmsahuri ya Taifa ya CCM Ndugu January Makaba imebainisha kuwa chama hicho kinafuatilia kwa karibu zoezi zima la uchaguzi nchini kote.
Tarifa hiyo imeongeza kuwa Mwana-CCM yoyote anayeshuhudia au kusikia mipango ya kuvunja amani na kuhujumu au kuvuruga zoezi la uchaguzi atume ujumbe mfupi kwenda nambari 15016, akielezea mahali alipo, tukio husika na ikiwezekana wahusika. Ujumbe huu ni bure. CCM itazishughulikia taarifa hizo na kuzipeleka kwa mamlaka husika.
Chama hicho pia kimesisitiza uchaguzi wa amani huku hadi sasa, katika sehemu kubwa ya nchi  dalili zote zinaonyesha kwamba upigaji kura umekuwa wa utulivu. Katika hatua nyingine  chama hicho kimewataka viongozi wote wa CCM kuwa macho dhidi ya hujuma kwa CCM katika vituo mbalimbali vya uchaguzi nchini kulekea kuhesabu kura na kutangaza matokeo.

Wednesday, 21 October 2015

Giroud,Mesut Ozil waimaliza Bayern,waipiga 2-0

Giroud,Mesut Ozil waimaliza Bayern,waipiga 2-0

Tarehe October 21, 2015

Olivier Giroud na Mesut Ozil wamegeuka mwiba kwa  Bayern Munich baada ya kuitandika mabao mawili kwa bila katika moja ya michezo ya klabu bingwa ulaya.
vikosi vilikua kama vifuatavyo

Arsenal

  • 33 Cech
  • 24 Bellerín
  • 04 Mertesacker
  • 06 Koscielny
  • 18 Monreal
  • 19 Cazorla
  • 34 Coquelin
  • 16 Ramsey (Oxlade-Chamberlain – 57′ )
  • 11 Özil
  • 17 Sánchez (Gibbs – 82′ )
  • 14 Walcott (Giroud – 74′ Booked )

Substitutes

  • 02 Debuchy
  • 03 Gibbs
  • 08 Arteta
  • 12 Giroud
  • 15 Oxlade-Chamberlain
  • 21 Chambers
  • 49 Macey

Bayern Munich

  • 01 Neuer
  • 21 Lahm
  • 17 Boateng
  • 27 Alaba
  • 18 Bernat
  • 14 Alonso (Kimmich – 70′ )
  • 25 Müller
  • 06 Thiago Alcántara
  • 23 Vidal (Rafinha – 71′ )
  • 11 Douglas Costa
  • 09 Lewandowski

Substitutes

  • 08 Javi Martínez
  • 13 Rafinha
  • 15 Kirchhoff
  • 16 Gaudino
  • 26 Ulreich
  • 29 Coman
  • 32 Kimmich
Ref: Cüneyt Çakir
Att: 49,824

Tuesday, 20 October 2015

Kagame afunguka Uchaguzi mkuu Tanzania

Kagame afunguka Uchaguzi mkuu Tanzania

Tarehe October 20, 2015
Rais wa Rwanda Paul Kagame pamoja na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake.
Rais wa Rwanda Paul Kagame ametoa ya moyoni kufuatia uchaguzi mkuu unataorajia kufanyika jumapili ya wiki hii huku dunia nzima ikielekeza macho na masikio nchini Tanzania.
Uchaguzi huo utahusisha makundi mbalimbali ya waangalizi wa Kimataifa takribani 600 waliowasili nchini pamoja na aliyekuwa Rais  wa Nigeria Goodluck  Jonathan aliyemaliza muda wake na kumuachia Rais  Muhammadu Buhari kwa amani suala linaloendelea kumpatia umaarufu kimataifa.
Kwa upande wake Rais wa Rwanda Paul Kagame kupitia moja ya ukurasa wake katika mitandao ya kijamii amezungumzia uchaguzi huo huku naye pia akiahidi kufuatilia kwa karibu uchaguzi huo ambao pia nchi za Afrika Mashariki  zinaufuatilia  kwa ukaribu.
“Kuhubiri kuhusu Demokrasia ni tofauti na utekelezaji wake, kama nchi za Afrika Mashariki zinashuhudia kinacho endelea nchini Tanzania katika uchaguzi mkuu.Tuna endelea kutazama kwa marafiki zetu ambao pia ni nchi yenye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwaonesha kwa vitendo Demokrasia ambayo itamtofautisha yeye na mimi  au na Rais Nkurunziza wa Burundi” Amesema Paul Kagame.
Aidha,nchi ya Burundi ilikumbwa na mchafuko kufuatia Rais Nkurunziza kuwania muhula wa tatu ambapo asilimia kubwa ya wananchi walikimbilia nchini Tanzania kuomba hifadhi kutokana na machafuko hayo.
Kagame, mwenye umri wa miaka 57, alichukua urais wa Rwanda mwaka 2003 aliposhinda kwa asilimia 95 ya kura. Alichaguliwa tena mwaka 2010 kwa muhula wa pili wa miaka saba kufuatia ushindi mkubwa.
Katika hatua nyingine ,Bunge la Rwanda limeitisha mjadala wa kujadili mabadiliko ya katiba ya nchi ili kumuwezesha Rais Paul Kagame wa nchi hiyo kuwania kiti cha urais kwa mara ya tatu mfululizo ifikapo mwaka 2017.
Kwa mujibu wa Maafisa wa serikali ya Rwanda walisema Kagame binafsi hataki kugombea muhula wa tatu lakini ni wananchi wanaotaka aendelee kubakia madarakani ili aendelee kudhamini uthabiti na ustawi wa kiuchumi.
Ujumbe wa Rais Kagame katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania huu hapa.

Mazishi ya Makaidi Yasitisha Kampezi za Ukawa nchi nzima

Mazishi ya Makaidi Yasitisha Kampezi za Ukawa nchi nzima

Tarehe October 20, 2015
Mgombea urais wa Ukawa Edward Lowassa pamoja na viongozi wengine wa Ukawa.
Mgombea urais kupitia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) amesitisha kampeni zake ngazi zote ili kutoa fursa kwa wananchi kuaga mwili wa aliyekuwa mwenyekiti mwenza, Dk. Emmanuel Makaidi.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tumaini Makene, , alisema usitishaji wa kampeni umelenga kuonesha heshima ya kipekee kwa Dk. Makaidi ambaye alijitoa muhanga katika kuimarisha UKAWA kwa hali na mali.
Amesema Dk. Makaidi, pia Mwenyekiti wa National League for Democracy (NLD) alichokianzisha mwaka 1992, na mgombea ubunge jimbo la Masasi mkoani Mtwara, alifariki dunia Alhamisi wiki iliyopita katika hospitali ya Nyangao, Masasi, baada ya kuugua ghafla ugonjwa wa shinikizo la damu (presha).
“Kesho (Leo) kuanzia saa tatu asubuhi tutakuwa viwanja vya Karimjee kwaajili ya kutoa heshima za mwisho kwa Dk. Makaidi, sambamba na hilo pia tutasitisha kampeni zetu za ngazi zote na katika shughuli hiyo viongozi wote wa kitaifa wa UKAWA pamoja mgombea Urais watakuwepo” alisema Makene.

Amesema baada ya mwili wa Dk. Makaidi kuagwa katika viwanja vya Karimjee, shughuli ya mazishi ya mwanasiasa huyo mkongwe aliyefariki akiwa na umri wa miaka 74 itahitimishwa katika makaburi ya Sinza jijini Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine amesema ratiba ya kampeni itaendelea Jumatano ya tarehe 21 Oktoba kwa mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa kwenda mkoani Morogoro kumalizia majimbo ambayo hakufika katika awamu yake ya kwanza ya kampeni mkoani hapo ambayo ni Kilombero, Mlimba, Mikumi, Ulanga Mashariki na Ulanga Magharibi.

JK afanya uteuzi mpya sekta ya Mahakama

JK afanya uteuzi mpya sekta ya Mahakama

Tarehe October 20, 2015
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt  Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi katika Mahakama kama ifuatavyo;
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi Premi Kibanga imebainsha kuwa Rais amemteua Bi. Katarina Revocati kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (Chief Registrar).  Kabla ya uteuzi huu,  Bi. Revocati alikuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani.
Rais pia  amemteua Ndugu John Rugalema Kahyoza kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani na kabla ya uteuzi huu, Ndugu Kahyoza alikuwa Msajili wa Mahakama Kuu.
Mwingine aliyeteuliwa ni Ndugu Ilvin Claud Mugeta ambaye anakuwa Msajili wa Mahakama Kuu. Kabla ya Uteuzi huu ndugu Mugeta alikua Mkurugenzi wa Ukaguzi na Maadili. Taarifa hiyo imebanisha kuwa uteuzi huu umeanza tarehe 3 Oktoba, 2015.

Friday, 16 October 2015

Tazara ‘Flyover’ kugharimu Bilioni 100


Tazara ‘Flyover’ kugharimu Bilioni 100




Barabara ya Juu ‘Flyover’ inavyotarajiwa kuwa ikikamilika.

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Japan, zimewekeana saini mkataba wenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 100, kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa barabara ya juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Mandela jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni mgombea wa Nafasi ya Urais kupitia Chama cha Mapinduzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameeleza kuwa fedha hizo zinatokana na msaada wa shilingi bilioni 93.438 kutoka Serikali ya Japan huku Serikali ya Tanzania ikichangia shilingi bilioni 8.26.
Mhe. Dkt. Magufuli ameongeza kuwa hatua hio ya utiaji saini ni faraja kubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam, kwa kuwa mradi huo wa ujenzi wa ‘flyover’ utasaidia katika kupunguza kero ya msongamano wa magari jijini.
Aidha amesema kuwa Serikali ya Japan imekuwa ikishirikiana kwa karibu sana na Serikali ya Tanzania, katika kuleta maendeleo kwa kufadhili miradi mbalimbali ya barabara na madaraja ikiwemo barabara ya Mwenge kwenda Tegeta, mradi uliogharimu shilingi bilioni 88, Mwenge kwenda Morocco ambayo ipo katika mkakati, pamoja na mradi wa ‘flyover’ wa Mbagala Rangi tatu kwenda Tazara.
Pia Mhe. Dkt. Magufuli ameeleza kuwa mkakati wa Serikali ni kuhakikisha inawaunganisha wananchi wake kupitia mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami, ili kurahisisha mawasiliano na usafirishaji wa watu, bidhaa na biashara kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale, ameeleza kufurahishwa na hatua hiyo ikiwa ni ishara na mwanzo wa kuleta maendeleao kwa wananchi wa Dar es Salaam, ambao wamekuwa wakisubiria kwa muda kuanza kwa mradi huo wa ‘flyover’ ya Tazara.
Amezidi kubainisha kuwa ujenzi wa mradi huo utafanywa na mkandarasi kutoka kampuni ya Sumitomo Mitsui Construction kutoka nchini Japan na utachukuwa muda wa miezi 35 kukamilka, ikifuatiwa na kipindi cha uangalizi kwa muda wa miezi 12 sawa na mwaka mmoja.
Kwa Upande wa Balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshida, amesema kuwa uhusiano wa Tanzani na Japan ni wa muda mrefu na kupitia mradi huu wa Flyover ya Tazara ni kielezo tosha cha kuendelea kuboresha uhusiano baina ya nchi hizo mbili, utakaosaidia kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania, pamaja na kukuza uchumi wa nchi na nchi jirani.

KAWA wabaini madudu kwenye Daftari la Wapigakura

KAWA wabaini madudu kwenye Daftari la Wapigakura


Moja ya jina katika Daftari la wapiga kura akionekana ni  mzungu na majina yake ambayo hayaeleweki.
Majina ya watu yalio andikwa  GGJGJHGHG GGHGGGHG.

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umebaini kuwepo madudu katika Daftari la kudumu la wapiga kura ikiwa ni siku kadhaa tangu Daftari hilo likabidhiwe kwa vyama vya siasa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Abdallah Safari pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, Reginald Munisi, walisema kumebainika kuna madudu na upungufu mwingi kwenye daftari na kudai kwamba daftari hilo haliaminiki.
“Tumeanza kulifanyia ukaguzi daftari la Tume baada ya kulipata  Jumatano, na kwa tuliyoyaona, sasa tumeelewa ni kwanini walikuwa hawataki kulitoa mapema,” alisema Prof. Safari ambaye ni wakili wa Mahakama Kuu nchini.
“… ni wazi Tume hii ambayo si tume huru imejiandaa kuhujumu uchaguzi kwa kuwa katika kituo kimoja tu tulichokagua tumeona majina feki mengi yakiwa yameingizwa,” aliongeza Munisi ambaye alisema ukaguzi ulifanywa katika jimbo la Dodoma mjini.

Dosari za msingi zilizobainika katika ukaguzi huo ni Majengo kuandikishwa kama wapiga kura. Katika hali ya kushangaza picha za majengo, ikiwemo migahawa zimeonekana kuwa ni sehemu ya majina ya wapigakura wa jimbo la Dodoma Mjini huku zikibeba majina ya watu na namba ya kitambulisho cha mpiga kura.
Baadhi ya vitambulisho kuonekana vikiwa na picha mbili: kumekutwa baadhi ya vitambulisho vinachoandamana na picha ya halisi za watu wengine nyuma.
Raia wa kigeni kuandikishwa: Kumekutwa majina ya wasiokuwa raia wa Tanzania wamejumuishwa kwenye daftari, majina mengine yakiwa yasiyoeleweka; picha za raia wanaoonekana kuwa wageni kama Wachina na Wazungu zimeonekana zikiwa sehemu ya wapigakura wa Tanzania; na majina yenyewe yana herufi tupu zisizo na irabu na hivyo kushindwa kusomeka. Kwa mfano limekutwa jina lililoandikwa LHPG SVWTN.
Picha za pikipiki kutokeza kama majina ya wapigakura: kumekutwa picha za pikipiki zikiwa ni sehemu ya majina ya wapigakura huku majina na picha hizo yakiwa na namba za vitambulisho vya wapigakura.
Majina yalioainishwa kuwa ni ya wanaume yana picha za wanawake: baadhi ya majina yalioneshwa kuwa ni ya kiume na kitambulisho kuonesha kuwa jinsia inayomiliki kitambulisho ni ya kiume lakini picha ni za wanawake.
Picha za wapigakura kupigwa katika maeneo tofauti ikiwemo sehemu zenye mabati na mbao badala ya kitambaa kimoja kilichokuwa kikitumiwa kwenye vituo vya Tume: picha za baadhi ya wapigakura zimeonekana kwa mwonekano tofauti wa nyuma (background), ikiwemo kupigwa kwenye sehemu za mabati na mbao hivyo kuzua hofu kuwa huenda uandikishwaji uliendelea katika maeneo mengine baada ya muda wa uandikishaji kumalizika.
Prof. Safari alisema kufuatia uchafu wa daftari, wanaandaa barua kwenda jumuiya za kimataifa ili kuzitahadharisha namna ambavyo serikali ya Chama Cha Mapinduzi inavyoshirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuvuruga uchaguzi.
“Leoleo tunaandika barua na kuzituma mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC, tunaipelekea pia Jumuiya ya Madola, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika pamoja na Umoja wa Mataifa kuwajulisha waone mbinu chafu za CCM kutafuta ushindi wa goli la mkono… wanajiandaa kuiingiza nchi katika machafuko,” alieleza Prof. Safari.
Munisi alisema wanaitaka tume ya taifa ya Uchaguzi kutoa majibu juu ya daftari hilo na kulirekebisha haraka sana kabla hawajatangaza uamuzi mwingine watakaouchukua iwapo hawataridhishwa na hatua za NEC.
Hadi leo ni siku tisa tu kabla ya Oktoba 25 ambapo Watanzania wapatao milioni 22 wanatarajiwa kujitokeza vituoni kupiga kura ya kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano, Wabunge na Madiwani.

Mwenyekiti Mwenza Ukawa Bw. Makaidi Afariki Dunia

Mwenyekiti Mwenza Ukawa Bw. Makaidi Afariki Dunia


Aliyekuwa Mwenyekiti Mwenza wa chama cha NLD Bw.Emmanuel Makidi.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa kupitia  chama cha NLD Bw.Emmanuel Makidi amefariki dunia leo mkoani Lindi katika Hospitali ya Nyangao.
Kwa mujibu wa  mke wake Bi Modesta Makaidi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Mwapachu arudisha kadi 2 CCM, atimkia kwa Lowassa


Mwapachu arudisha kadi 2 CCM, atimkia kwa Lowassa




Balozi Juma Mwapachu .
Balozi Juma Mwapachu ambaye  ni mmoja kati ya wanachama wakongwe wa Chama cha Mapinduzi (CCM),amerudisha rasmi kadi ya chama cha Mapinduzi na ile ya TANU katika ofisi za CCM kata ya Mikocheni jijini Dar es Salaam leo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mtandao huu, Mwapachu amesema kwamba ameamua kurudisha kadi ya CCM kutokana na kutokukubaliana na uamuzi wa CCM wa kumkata mwanasiasa ambaye angeweza kuleta mabadiliko ndani ya CCM Edward Lowassa, ambaye ni Mgombea urais wa kupitia Ukawa hivisasa.
Aidha,Mwapachu  ambaye alikuwa  Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema baada ya kurudisha kadi hizo anaungana na UKAWA ambapo mara baada ya uchaguzi mkuu ata amua ni chama gani aungane nacho.
Akizungumzia kuhusu wanaohama kutoka CCM kubezwa na kuitwa Makapi, Mwapachu amesema kwamba waliobaki CCM ndio Makapi kwa madai kuwa chama cha Mapinduzi kimepoteza mwelekeo na kuwa ni chama kinachotegemea maamuzi ya watu wachache.
Amesema hivisasa yeye ni Mwanaharakati, akidai kwamba mabadiliko ya msingi zaidi ni Katiba, lakini chama cha Mapinduzi toka mfumo wa vyama vingi uanze, CCM katika uongozi wake imeendelea kutojali uwepo wa vyama vingine licha ya kuwa nchi ipo katika mfumo wa vyama vingi.
Ameongeza kuwa CCM wameendelea kuhodhi madaraka na kujiona kama ni chama cha  kutawala nchi hii milele yote na  kwamba wakati sasa umefika kwa  wananchi ambao asilimia kubwa ni vijana kuwa wanataka mabadiliko.

Amesisitiza kuwa asilimia 65 ya wananchi hivisasa ni vijana chini ya miaka 30, ambao wanataka mabadiliko ya haraka ambayo yatawapa ajira na kuwapa nafasi nzuri ya kuendesha maisha yao lakini hayo yote hawaja yaona.
Katika hatua nyingine amesema amekuwa akikutana na wanafunzi mbalimbali wa vyuo vikuu, ambao wamekuwa wakihoji kwa nini wanasiasa ndani ya chama hicho wameshindwa kuwaletea wananchi maendeleo,  huku wakionekana kujinufuisha wao wenyewe ikiwa ndio msingi hasa wa mabadiliko wanayo yataka.

Saturday, 10 October 2015

Fahamu machache ya aliyekaimu nafasi ya Blatter FIFA,Hayatou

Fahamu machache ya aliyekaimu nafasi ya Blatter FIFA,Hayatou

Tarehe October 10, 2015
Issa Hayatou

Ni habari ambazo wengi wamezifurahia na hasa Afrika, lakini kiongozi wa soka barani Afrika Issa Hayatou huenda binafsi alikuwa akiogopa kutajwa kiongozi wa Fifa.
Kwa miaka 111 tangu kuanzishwa kwa Fifa, shirika hilo linalosimamia soka duniani sasa linaongozwa na Mwafrika.
Lakini Hayatou amekuwa mtu ambaye hapendi kuangaziwa sana na vyombo vya habari.
Lakini sasa, mzee huyo anayependa sana kuongoza akiwa amejifungia afisini, hataweza kukwepa wanahabari.
Kwa siku 90 zijazo, Sepp Blatter atakapokuwa amesimamishwa kazi, macho yote yatakuwa kwa raia huyo wa Cameroon na labda hata zaidi kutokana na kashfa inayokumba shirikisho hilo.
Hayatou alizaliwa kaskazini mwa Cameroon, akiwa mwana wa mmoja wa masultan wa eneo hilo. Kakake alikuwa waziri mkuu wan chi hiyo wakati mmoja.
Kama Blatter, Hayatou ni mwanasiasa mwenye uwezo wa kukabiliana na changamoto kwa ustadi.


Shambulio dhidi ya timu ya Togo
Wakati wa ujana wake, alikuwa mchezaji. Hayatou, 69, amekuwa makamu wa rais wa Fifa, mwanachama wa kamati tendaji ya shirikisho hilo tangu 1990, na amekuwa akiongoza soka Afrika tangu 1988.
Jinsi Caf ilivyoshughulikia shambulio lililotekelezwa dhidi ya timu ya Togo wakati wa michuano ya Kombe la Taifa Bingwa Afrika 2010 inaashiria sifa za Hayatou.
Alikataa kufichua hatua zilizochukuliwa na Caf kushughulikia mzozo huo kwa sababu hakudhani ilikuwa muhimu kwa umma kujua hilo. Ukweli ni kwamba, aliabiri ndege usiku na kwenda hadi huko kutatua mzozo uliotokea.
Kutokana na ukosefu wa habari kuhusu hatua alizochukua, wengi walikosoa Caf wakidhani ilinyamaza.
Caf ilijibu hatua ya Togo kujiondoa kutoka kwa dimba hilo kwa kuipiga marufuku kwa miaka miwili. Uamuzi huo hata hivyo ulibatilishwa kupitia juhudi za Mahakama ya Utatuzi wa Mizozo ya Michezo na Blatter mwenyewe.
Hayatou, aliyekuwa mkurugenzi wa soka Cameroon katikati mwa miaka ya 1980 bila shaka atakabiliwa na maswali mengi atakapokutana na wanahabari mara ya kwanza.
Mitandao ya kijamii tayari imeanza kufufua madai yaliyokuwepo dhidi ya Hayatou awali, madai ambayo ameyakanusha.

Kubadilisha sheria za Caf
Moja ya haya ni kushutumiwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki 2011 kwa madai kwamba alipokea kiinua mgongo kutoka kwa kampuni ya matangazo ya michezo ya ISL kati ya 1989 na 1999.
Kwa mujibu wa IOC, Hayatou alikiri kupokea malipo hayo, akisema ilikuwa zawadi kwa shirikisho lake.
Kisha, kulikuwa na madai, yaliyosikika na wabunge wa Uingereza katika kamati ya utamaduni, vyombo vya habari na michezo ya Bunge la Commons mwaka 2011, kwamba Hayatou alipokea hongo kuhusiana na utoaji wa haki kwa Qatar kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia 2022, madai ambayo ameyakanusha.
Mapema mwaka huu, alisimamia kubadilishwa kwa sheria za shirikisho hilo kuhusu umri ndipo aweze kuendelea kuongoza.
Maafisa wa Caf walikuwa wakistaafu wakitimiza miaka 70, lakini hilo lilibadilishwa Aprili wanachama wote walipounga mkono kuondoa sheria hiyo.
Hii ina maana kwamba Hayatou, aliye na umri wa miaka 69 sasa, anaweza kuwania tena muhula wake ukimalizika 2017.
Sheria pia zilikuwa zimebadilishwa kupunguza nguvu za wapinzani wa Hayatou.
Caf ilipitisha sheria kwamba rais anaweza tu kutoka kwa wanachama wa kamati tendaji, ambao wengi ni washirika wa Hayatou.
Hilo lilizuia raia wa Ivory Coast Jacques Anouma kumpinga.
Lakini mashabiki wake watataja ustawi wa soka Afrika kama ishara ya utendakazi wake.
  • Alipigania kuongezwa kwa nafasi za wawakilishi wa Afrika Kombe la Dunia kutoka wawili hadi watano.
  • Alipigania kuanzishwa kwa mfumo wa mzunguko katika uenyeji wa Kombe la Dunia katika Fifa hatua ambayo mwishowe ilipelekea Afrika Kusini kuwa taifa la kwanza kuandaa Kombe la Dunia Afrika 2010.
  • Aliongeza mara dufu timu zinazoshiriki Kombe la Taifa Bingwa Afrika kutoka nane hadi 16.
  • Alianzisha shindano la vijana la chini ya umri wa miaka 20 na chini ya miaka 17.
  • Alibadilisha muundo wa Kombe la Taifa Bingwa Afrika na Ligi ya Klabu Bingwa Afrika miaka ya 1990, na pia kuanzisha ligi ya daraja la pili kwa klabu.
  • Alitekeleza dimba la bingwa wa Afrika kwa wanawake.
  • Aliimarisha sana uwezo wa kifedha wa Caf.
Hayatou, ambaye anaugua maradhi ya figo, na huhitaji kusafishwa damu mara kwa mara, kwa sasa yuko mji mkuu wa Cameroon, Yaounde na anatarajiwa kusafiri kwenda makao makuu ya Fifa mjini Zurich karibuni.
Amesema hatawania uchaguzi wa Februari lakini atasaidia kufanikisha mageuzi katika shirikisho hilo.
Alikuwa amejaribu kumng’oa Blatter katika uongozi wa Fifa uchaguzini 2002 lakini akashindwa.
Kwake, ushauri kwamba unafaa kuwa makini katika unalojitakia unafaa sana.

Klopp asema kuifunza Liverpool ni changamoto

Klopp asema kuifunza Liverpool ni changamoto

Tarehe October 10, 2015
Jurgen Kloppiverpol

Mkufunzi mpya wa timu ya Liverpool Jurgen Klopp ameitaja kazi yake mpya katika kilabu hiyo ya Anfield kuwa changamoto kubwa katika kandanda duniani.
Raia huyo wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 48 aliteuliwa kuchukua mahala pake Brendan Rodgers na hivyobasi kuweka saini kandarasi ya miaka 3 yenye thamani ya pauni milioni 15.
Anachukua kikosi ambacho kiko katika nafasi ya 10 katika jedwali la ligi ya Uingereza kikikiwa na alama 12 kutoka kwa mechi nane.
”Mimi sio mtu wa kukabiliana na mambo rahisi ”,Klopp aliambia runinga ya Liverpool .”Hii ndio changamoto kubwa katika soka.Ni kazi ilio na mvuto zaidi katika soka duniani”..

Matukio katika picha mkutano wa Lowassa Moshi

Matukio katika picha mkutano wa Lowassa Moshi

Tarehe October 10, 2015
Mkutano wa Kampeni za Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa, Katika Uwanja wa Isanja, Kata ya Nasai, Jimbo la Siha.
Maelfu ya wananchi jana walihudhuria mkutano wa kampeni wa Umoja wa katiba ya Wananchi Ukawa ulio ongozwa na mgombea urais wa Ukawa Edward Lowassa katika maeneo ya Karatu na Siha mkoai Kilimanjaro.
Hivi ndivyo hali ilivyokuwa,

Magufuli awanadi Ridhiwani, Kawambwa mkoani Pwani


Magufuli awanadi Ridhiwani, Kawambwa mkoani Pwani

Tarehe October 10, 2015

Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akimnadi mgombea ubunge wa jimbo jimbo la Chalinze Ndugu Ridhiwani Kikwete.
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli ameipongeza wilaya ya Bagamoyo kufuatia kugulika kwa gesi ambayo itasaidia kukuza uchumi hapa nchini wakati akiwanadi wanasiasa Ridhiwani Kikwete pamoja na Shukuru Kawambwa.
Akizungumza katika mikutano yake ya kampeni iliyofanyika katika majimbo ya Chalinze na Bagamoyo Magufuli alibanisha kuwa ugunduzi wa gesi hiyo itasaidia ujenzi wa viwanda katika serikali yake.
Kwa upande mwingine Magufuli  alisema serikali yake anatarajia iwe ya viwanda ili kutoa fulsa ya ajira kwa vijana ambao wamekuwa hawana kazi mara baada ya kumaliza masomo yao.

Mgombea urais TLP, afunguka Mrema kumnadi Magufuli


Mgombea urais TLP, afunguka Mrema kumnadi Magufuli


Tarehe October 9, 2015
Mgombea urais kupitia chama cha TLP Macmillan Lyimo.
Mgombea urais kupitia chama cha TLP Macmillan Lyimo amefunguka kufuatia Mwenyekiti wa chama chake cha TLP Augustine Mrema kumnadi mgombea wa Chama cha Mapinduzi Dkt.John Pombe Magufuli wakati naye pia ni mgombea urais. Akizungumza na kituo kimoja cha redio Lyimo amesema kwamba hayo ni maamuzi yake binafsi na kwamba kauli hiyo haijatolewa na mkutano wowote wa chama, bali ni maoni binafsi akisisitiza kuwa alilofanya Mrema si jipya wa la ajabu.
“Hili jambo siyo la ajabu, hata Marekani, Colin Powell alitangaza kumuunga mkono Obama licha ya kuwa chama tofauti pia uamuzi wake haunipi shida. Amesema Macmillan Lyimo
Alipoulizwa mahusiano kati yake na mwenyekiti huyo, Lyimo amesema kuwa mahusiano ndani ya chama hicho ni mazuri na hakuna ugomvi wowote.
Akizungumzia kampeni za uchaguzi pamoja na wagombea urais Lyimo amesema yeye ndiye atakayeshinda urais mwaka huu, na kamwe Rais hatoki CCM.
Mwenyekiti wa chama cha Siasa cha TLP Augustino Mrema akiwa na mgombea urais wa CCM Dkt,John Pombe Magufuli.

Mosore ageuka Mbogo NCCR-Mageuzi, agoma kung’oka

Mosore ageuka Mbogo NCCR-Mageuzi, agoma kung’oka

Tarehe October 9, 2015
Makamu Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi (Bara), Leticia Ghati Mossore.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi Leticia Mosore amegeuka mbogo kufuatia kugoma kuong’olewa madarakani kama ilivyotangazwa na Mwenyekiti wa chama hicho James Mbatia hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Mosore amepinga vikali madai ya mwenyekiti wa chama hicho James Mbatia kwamba anatumika na chama cha Mapinduzi kwa ajili ya kukibomoa chama chao ambacho ni mshirika mkubwa wa umoja wa katiba ya wananchi UKAWA.
Mosore amesema kwamba madai ya kutumika hayana ukweli wowote ukilinganisha na madai yake kwamba chama chao kimepewa majimbo machache pamoja na Mwenyekiti wake kuonekana anaegemea sana katika kutekeleza majukumu ya ukawa na kukitelekeza chama cha NCCR-Mageuzi.

Katika hatua nyingine Mosore amemshangaa Mbatia kusema kuwa ametumika wakati yeye aliteuliwa ubunge wa viti maalumu na Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akihoji ni kipi zaidi alicho kifanya hadi kufikia chama cha Mapinduzi kumzawadia nafasi hiyo nyeti ya ubunge.

clouds stream