Visiwa vya Guam,Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson amesema kuwa hakuna tishio lolote la hivi karibuni kutoka Korea Kaskazini , licha ya Pyongyang kusema kuwa inapanga kushambulia eneo la Guam nchini Marekani.
Tillerson pia amemtetea Rais, Donald Trump ambaye ameitishia Korea Kaskazini kwamba ataikabili kivita na kudai kuwa Rais Trump alitaka kutuma ujumbe kwa Korea Kaskazini.
Katika ujumbe wa mtandao wa Twitter uliochapishwa Alfajiri, Rais Trump amesema kuwa silaha za kinyuklia za Marekani zimeimarika zaidi ya ilivyokuwa awali lakini akasema kuwa anatumai hatalazimishwa kuutumia uwezo huo.
Ujumbe huo wa Twitter unafuatia kuzuka mwa majibizano kati ya pande hizo mbili huku kisiwa hicho cha Guam ambacho ndio makao ya ndege za kivita za Marekani na watu 163,000 kikizungumziwa.
“Huku idara yetu ya maswala ya kigeni ikifanya kila juhudi ya kutatua swala hilo, kwa njia ya kidiplomasia ni lazima ifahamike kwamba Jeshi la Marekani limeimarika na lina ulinzi mkali duniani,” imesema sehemu ya Twitter hiyo.