Monday 14 August 2017

Uchaguzi Kenya: Raila Odinga awashauri wafuasi wa upinzani kususia kazi Jumatatu

Raila Odinga Kibera, Nairobi, Kenya Agosti 13, 2017

IMG-20170426-WA0006

Bw Odinga alikariri madai yake ya awali kwamba serikali ya Bw Kenyatta iliiba kura, ingawa waangalizi wa uchaguzi wamesema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki

Kinara wa muungano upinzani nchini Kenya Raila Odinga, amewashauri wafuasi wake kususia kazi siku ya Jumatatu kama njia ya kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumanne iliyopita.

Akihutubia wafuasi wake mtaani Kibera, Nairobi kwa mara ya kwanza kabisa tangu kutangazwa matokeo, ambapo Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi, Bw Odinga amedai kuwa serikali ilikiwa imepanga kuwaua wafuasi wa upinzani kabla ya kutangazwa matokeo.

Hii ni siku moja baada wa watu kadha kuripotiwa kuuawa maeneo tofauti ya mji wa Nairobi na Kisumu, wakati wafuasi wa upinzani walijitokeza kulalamikia matokeo ya uchaguzi

Wafuasi wa upinzani wakiandana mtaa wa Mathare Nairobi
Wafuasi wa upinzani wakiandana mtaa wa Mathare Nairobi

Aidha Odinga amesema kuwa siku ya Jumanne, mrengo wa Nasa utatangaza mwelekeo ambao utachukua.

Bw Odinga baadaye alizuru mtaa wa Mathare Kaskazini jijini Nairobi ambapo msichana wa miaka tisa alifariki baada ya kupigwa risasi wakati wa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji.

Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mashindi kwa kura 8,203,290 huku naye Raia Odinga akipata kura 6,762,224.

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, ambaye alikuwa mpatanishi mkuu baada ya mzozo wa kisiasa nchini Kenya miaka kumi iliyopita, alikuwa ametoa wito kwa Bw Odinga kutumia mifumo ya kisheria kutafuta haki kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais.

Raila Odinga
Wafuasi wengi wa Bw Odinga walihudhuria mkutano huo uwanja wa Kamukunji mtaa wa Kibera, Nairobi
Polisi wa kupambana na ghasia mjini Kisumu
Polisi wa kupambana na ghasia mjini Kisumu

Bw Annan alikuwa mpatanishi mkuu baada ya ghasia kuzuka baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 uliokumbwa na utata.

"Namshukuru kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kampeni ya uchaguzi ya amani aliyoiendesha. Amekuwa mtetezi jasiri wa demokrasia," amesema Dkt Annan kupitia taarifa.

"Kwa hivyo, namhimiza sasa afuatilie malalamiko yake kupitia mifumo ya kisheria iliyowekwa na aweke maslahi ya taifa mbele, kama alivyofanya kwa uzalendo mara nyingi awali."

Mwaka 2007, watu zaidi ya 1,000 walifariki na wengine 600,000 wakafurushwa makwao wakati wa ghasia za kikabila zilizozuka baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.

clouds stream