Kura zinaendelea kuhesabiwa na matokeo kutangazwa baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya Jumanne.
Katika matokeo yaliyokuwa yametangazwa kufikia saa tatu asubuhi Jumatano, Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee alikuwa akiongoza akiwa na kura 7,461,933 (54.64%) akifuatwa na Raila Odinga wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) aliyekuwa na kura 6,079,136 (44.51%). Matokeo hayo ni ya vituo 36659 kati ya 40,883.
Kura ambazo zilikuwa zimeharibika kufikia wakati huo ni 353,389.
Muungano wa Nasa umepinga matokeo yanayoendelea kutangazwa na tume hiyo na kusema si sahihi.
Bw Odinga amesema IEBC imefanya makosa kwa kutangaza matokeo hayo bila kuwaonyesha maajenti wa vyama Fomu 34A, kubainisha matokeo hayo yametoka katika vituo gani.
Katika baadhi ya vituo, shughuli ya upigaji kura ilichelewa kuanza na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) iliongeza muda kufikia wakati uliokuwa umepotezwa kabla ya kufungua vituo.
Kisheria, vituo vilitakiwa kufunguliwa saa kumi na mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na moja jioni saa za Afrika Mashariki.
Lakini katika baadhi ya maeneo, mvua kubwa ilitatiza uchukuzi na upigaji kura na kwingine hitilafu za kimitambo zikachangia kukwamisha upigaji kura. Muda wa kufungwa kwa vituo uliongezwa kwa vituo vilivyochelewa kufunguliwa.
Wengi wanahofia uwezekano wa kutokea tena kwa ghasia za baada ya uchaguzi sawa na ilivyotokewa baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Watu zaidi ya 1,100 walifariki na wengine 600,000 kuachwa bila makao.
Tume ya uchaguzi imetangaza matokeo kutoka kwa vituo 36659 kati ya jumla ya vituo 40883 ambapo:
Uhuru Kenyatta wa Jubilee ana kura 7,461,933 (54.64%)
Raila Odinga wa ODM kura 6,079,136 (44.51%)
Joseph Nyagah (huru) 33,710 (0.25%)
Abduba Dida wa ARK 29,411 (0.22%)
Ekuru Aukot wa Thirdway Alliance 23,976 (0.18%)
Japheth Kaluyu (huru) 10,316 (0.08%)
Cyrus Jirongo wa UDP 10,019 (0.07%)
Michael Wainaina (huru) 7,919 (0.06%)
Kura zilizoharibika kufikia sasa ni 353,389
Ili kushinda, mgombea urais anahitajika kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa, na angalau asilimia 25 katika kaunti 24 kati ya kaunti 47 nchini humo.
Iwapo hakuna mgombea atakayetimiza hilo, basi uchaguzi wa marudio utafanyika katika kipindi cha siku 30.
Kujitokeza mapema
Wapiga kura walianza kujitokeza alfajiri na mapema kupiga kura.
Foleni ndefu zilishuhudiwa katika vituo vingi, na kwingine visa vya watu kuumia katika mkurupuko wa kupanga foleni vituo vilipofunguliwa viliripotiwa.
Katika baadhi ya vituo, kuliripotiwa pia visa vya mitambo ya kuwatambua wapiga kura kufeli.
Katika moja kati ya vituo vinne nchini humo, maafisa wa IEBC walikuwa wamesema kwamba hakuna huduma nzuri ya mtandao maana kwamba wasimamizi wa uchaguzi katika vituo hivyo watahitaji kusafiri hadi ameneo yenye huduma nzuri ya simu kutuma matokeo kikamilifu.
Kumekuwa pia na taarifa kwmaba mwanamume mmoja ameuawa katika makabiliano kati ya wafuasi wa wagombea wawili katika kaunti ya Kilifi, pwani ya Kenya.
Lakini kulikuwa na kisa cha kutia moyo pale mwanamke mmoja alipojifunzua mtoto msichana alipokuwa kwenye foleni akijiandaa kupiga kura Pokot Magharibi.
Pauline Chemanang alisema kujifungua kwake ni baraka na akampa mtoto wake jina Kura, kwa mujibu wa kituo kimoja cha redio.
Rais Kenyatta, baada ya kupiga kura yake kituo cha Mutomo eneo lake la nyumbani la Gatundu, kaskazini mwa Nairobi, alisema kwamba yuko tayari kukubali matokeo ya uchaguzi huo.
"Kwa wapinzani wangu, kama nilivyosema mara nyingi awali, ikitokea kwamba washindwe, basi hebu tukubali uamuzi wa wananchi. Nina nia, mwenyewe, kukubali nia ya wananchi," amesema.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga alipiga kura yake katika mtaa wa Kibera, Nairobi.
Akiongea nje ya kituo hicho, aliwahimiza wafuasi wake: "Hebu tujitokeze kwa wingi na tupige kura."
Mwangalizi mkuu wa Umoja wa Ulaya Marietje Schaake amesema itategemea sana imani ya wananchi katika mfumo mpya wa kiteknolojia wa kupiga kura.
Kabla ya siku ya uchaguzi, meneja wa masuala ya teknolojia katika IEBC Chris Msando aliuawa na watu wasiojulikana.
Kulikuwepo na madai ya kwamba huenda kukawa na wizi wa kura na pia katika baadhi ya maeneo taarifa za kueneza kwa karatasi zenye ujumbe wa chuki zilizagaa.
Siku chache kabla ya uchaguzi, Wakenya wengi walikuwa wakinunua chakula na maji na kujihifadhia wakihofia hali baada ya uchaguzi.
Polisi pia walifanya mipango ya kushughulikia dharura iwapo ghasia zingetokea.