Wednesday, 2 August 2017

Serikali Yaja Na Mpango Maalum Kupunguza Matumizi Ya Mkaa Na Kuni

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.
IMG-20170426-WA0006

Serikali imesema kuwa utaratibu umeandaliwa ili kuhakikisha watu wanatumia gesi kama nishati mbadala ya kuni na mkaa kwa ajili ya kuhifadhi mazingira.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia Muungano na Mazingira, January Makamba katika mkutano na waandishi wa habari na kuelezea nia ya Serikali ya kuhamia katika nishati mbadala kwa matumizi ya kawaida.

Waziri Makamba amesema kuwa ili kudhibiti uharibu wa mazingira unaosababishwa na ukataji wa miti ambayo hutumika katika kuchoma mkaa na kuni, Serikali imeandaa mpango maalum kwa Mashirika ya Umma kuachana na matumizi ya mkaa na kuni na badala yake yatumie gesi.

“Asilimia 90 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa kama nishati ya kupikia na mwanga, na hivyo matumizi ya mkaa yameongezeka kwa kiasi kikubwa nchini na kutishia ustawi wa misistu na vyanzo vya maji nchini,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa Dar es Salaam pekee, wastani wa tani 500,000 za mkaa zinatumika kila mwaka, huku taasisi za Umma za Serikali kama hospitali, magereza, kambi za jeshi na mashule wakiwa vinara wa matumizi ya mkaa na kuni.

“Nimefikia makubaliano na wauzaji na wasambazaji wa gesi nchini ili kusimika mitambo ya kuhifadhi gesi na majiko ya kupikia kwa kutumia gesi katika taasisi zote za umma ili Serikali iwe kinara katika kuleta mageuzi hayo,” amesisitiza Waziri Makamba.

clouds stream