Familia Ya Msemaji Jeshi La Kenya Yatoa Neno Baada Ya Kuripotiwa Kutoweka
Saa chache baada ya Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Kanali, Joseph Owuoth kuripotiwa kutoweka na kutojulikana mahali alipo, familia yake imeibuka na kudai kuwa mtu huyo yupo salama na hajafukuzwa kazi.
Mapema leo, taarifa zilizagaa ya kuwa Kanali huyo alitoweka ghafla alipokuwa akiwasiliana na dada yake aliyetambuliwa kwa jina la Elizabeth kabla ya kukatika ghafla kwa mawasiliano ya simu akiwa katika eneo linalodhaniwa kuwa ni Nakuru.
Kiongozi huyo wa Jeshi amewahi kukiri kuwa Jeshi hilo linaendesha mafunzo maalum kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, huku zikiwa zimepita wiki mbili tu tangu Muungano wa Upinzani (NASA) kuibua tuhuma nzito zinazolihusisha jeshi hilo na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 8, mwaka huu.
Tetesi za kutoweka kwa Kanali Owuoth zimeibuka ikiwa ni siku chache tu zimepita tangu Mtaalam wa Teknolojia wa Tume ya Uchaguzi Kenya (IECB), Chris Muhando kuripotiwa kutoweka na siku chache baadae mwili wake kukutwa katika chumba cha kuhifadhia maiti, huku mkono wake mmoja ukiwa umekatwa.