Polisi Watangaza Kiama Kwa Wapiga Debe Dar Es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda maalumu ya Dares salaam limetangaza oparesheni maalum katika vituo vyote vya daladala siku ya Jumatatu kwa ajili ya kuwaondosha wapiga debe.
Uamuzi huo unafuatia kushamiri vitendo vya wizi na uporaji wa mali za abiria katika vituo vya daladala vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watu wanaojulikana kwa jina la wapiga debe.
Kwa mujibu wa Kaimu kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es salaam Lucas Mkonya amesema wananchi wengi wamekua wakipeleka malalamiko juu ya wizi huo unaotokea kwenye vituo vya daladala unaofanywa na baadhi ya wapiga debe kwenye vituo.
Ni matumani ya wananchi kuwa Operesheni hiyo itazaa matunda kufuatia kukithiri vitendo vya wizi vinavyofanywa na wapiga debe ambao asilimia kubwa ni mateja.
Utafiti wa mtandao huu unaonesha kuwa wezi wamekua wakishirikiana na baadhi ya makondakta wa daladala kuwaibia abiria.
Wezi wamekua wakipanda katika daladala na kuiba kisha kushuka bila kutozwa nauli na makondakta suala linaloashiria kuwa wanafahamiana.