Tarehe July 26, 2016
Wabunge 2 wa Chadema wako matatani kufuatia kuitwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha na kutakiwa kuripoti kwa RCO kufuatia madai ya kufanya mikutano ya kisiasa suala ambalo limepigwa marufuku.
Wabunge walioitwa kwa mahojiano ni mbunge wa Karatu,Wilbroad Qambalo na mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Arusha, Cecilia Paresso.
Mwingine aliyeitwa ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Karatu, Jubilate Mnyenye na Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Karatu, Lazaro Bajuta wote wanadaiwa kupuuza agizo la kutofanya mikutano ya hadhara katika jimbo hilo.
Wakizungumza jana baada ya kukabidhiwa barua za wito wa polisi, Qambalo na Paresso walisema wamestuka kutakiwa kuripoti ofisi ya Mkuu wa upelelezi mkoa wa Arusha jumatano.
Parreso alisema, walipokea barua jana saa sita mchana na kutakiwa kuripoti kwa RCO, saa nane lakini wakampigia na kumweleza wana ratiba nyingine tayari waende jumatano na akakubali.
Katika hatua nyingine Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkombo alipotakiwa kuelezea agizo hilo alisema yupo likizo.
Marufuku ya mikutano ya kisiasa imeendelea kuvikumba vyama vya Upinzani licha ya Jeshi la Polisi kusema kwamba halijapiga marufuku mikutano hiyo ya kisiasa.