Tarehe July 12, 2016
Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limedhamiria kwenda Mkoani Dodoma kuzuia mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliopangwa kufanyika Mjini humo kwa madai ya kulisaidia Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya kisiasa licha ya kutotakiwa kufanya hivyo na mwenyekiti wa chama hico, Freeman Mbowe.
Kiongozi mmoja mwandamizi wa BAVICHA Makao Makuu aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake amesema, uamuzi wa wao kwenda Dodoma uko palepale.
Tumeshaamua kwenda Dodoma na hakuna yeyote anayeweza wa kutuzuia na uamuzi wetu uko palepale na tutatekeleza kila ambacho tumepanga,” amesema.
Mkutano Mkuu wa CCM umepangwa kufanyika mkoani Dodoma wiki mbili zijazo ambapo pamoja na mambo mengine Rais, Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kukabidhiwa rasmi uenyekiti wa taifa wa chama hicho.
Msimamo mkali wa kiongozi huyo wa BAVICHA umefuatia uamuzi wa mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, na Kada Maarufu wa chama hicho, Waziri Mstaafu Edward Lowassa kuwaasa vijana wa Chadema kutokwenda Dodoma kukabiliana na CCM.
Mbowe alitoa kauli hiyo siku ya Jumapili, kufuatia kuwapo kwa taarifa kuwa jeshi la polisi nchini, limeapa kupambana na viongozi na wafuasi wa Chadema, ikiwa watafika mkoani humo kuzuia mkutano wa CCM.
Chadema kimeamua kuchukua hatua ya kukabiliana na CCM baada ya jeshi la polisi kuzuia mikutano ya ndani ya chama hicho, mikutano ya hadhara na mahafali yaliyopangwa kufanywa na Umoja wa Wanavyuo wa Chadema (CHASO), katika baadhi ya mikoa.
Kauli ya Mbowe imepingwa na baadhi ya vijana katika maeneo mbalimbali, ikiwamo mkoani Arusha, ambako uongozi wa mkoa umekabidhi kwa BAVICHA kiasi cha Shilingi milioni 5 kwa ajili ya kwenda Dodoma.
Miongoni mwa mahafali ya Chadema yaliyovurumishwa na polisi, ni pamoja na yale yaliyofanyika Mkoani Dodoma ambako mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.