Tarehe July 12, 2016
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameagiza wenyeviti wa halmashauri 18 nchini zinazoongozwa na Ukawa kuacha utaratibu wa kutoa fedha za halmashauri kuwasaidia mafuta ya magari Wakuu wa Wilaya au kuzitumia kwa ajili ya masuala ya kisiasa ya vyama vyao.
Akizungumza na Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri zinazoongozwa na Ukawa katika mkutano uliofanyika Mjini Arusha, Mbowe alisema viongozi hao wanapaswa kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa na halmashauri hizo zinatumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Amesema wametambua kuwa kuna matumizi mabaya ndani ya Serikali, mbali na wafanyakazi hewa ambao wapinzani wamekuwa wakilalamika tangu mwaka 2005.
“Bado kuna halmashauri ambazo zimekuwa zikitumia fedha kufadhili ofisi za wakuu wa wilaya na chama tawala, jambo ambalo sasa kwa halmashauri za Ukawa halitakuwapo,” amesema.
Ameongeza kuwa maeneo ambayo wakuu wa wilaya wamezoea kuomba fedha za mafuta na CCM wamekuwa wakiomba fedha kwa ajili ya kazi zao tunawaambia wasithubutu tena kwenda kwenye halmashauri zinazoongozwa na Ukawa, kwani hatutawapa fedha na tunawaumbua.
Mbowe amesema katika halmashauri za Ukawa hawataki kusikia kuna fedha zimetolewa kwa wakuu wa wilaya au chama chochote cha siasa.
Amesema wamekubaliana kuanzisha mipango mikakati ambayo itawezesha kubuniwa vyanzo vipya vya mapato ambavyo ni rafiki kwa wananchi, kupatikana kwa ajira na kuboresha huduma muhimu za Watanzania.
Akizungumza baada ya maelekezo hayo, Mwenyekiti wa Madiwani Chadema nchini ambaye pia ni Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro amesema watatekeleza na hawatakubali kuingiliwa na wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na makatibu tawala.
Calist alisema katika halmashauri za Ukawa uamuzi wa mwisho wa uendeshaji wa halmashauri utafanywa na madiwani na siyo mtu kutoka nje ya halmashauri hizo.
“Tutasimama na kutetea mamlaka ya kisheria ya Serikali za mitaa hapa nchini,” amesema.
Katibu wa Madiwani wa Ukawa nchi nzima ambaye ni Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob amesema watahakikisha wanasimamia utendaji mzuri wa halmashauri zote wanazoziongoza ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.