Askari Wengine Watatu Wauawa Marekani
Tarehe July 18, 2016
Katika hali ya kushangaza askari polisi watatu leo wameuawa kwa kupigwa risasi nchini Marekani katika eneo la Baton Rouge huku mmoja wa wahanga hao akiwa askari mweusi aliyefahamika kama Montrell Jackson.
Haya yanatokea ikiwa ni wiki moja tu imepita tangu askari wengine wanne kuuawa kwa kupigwa risasi na kuwaacha wengine wakiwa wamejeruhiwa vibaya huko Jijini Dallas,katika maandamano ya watu weusi wakipinga vitendo vya askari polisi nchini humo hasa weupe kuwaua watu weusi.
Akizungumzia mauaji hayo Rais wa Marekani, Barack Obama amesema mauaji hayo ni kazi ya watu waoga ambao hawafanyi hivyo kwa ajili ya watu watu wengine na kudai kuwa hakuna maelezo ya kueleweka kwa vitendo vya vurugu na mauaji dhidi ya utekelezaji wa sheria.
Tukio hili la kutisha ni la nne sasa kutokea nchini Marekani yakihusisha maafisa wa polisi ndani ya muda wa wiki mbili zilizopita. Matukio hayo tayari yameacha vifo vya watu 12, wakiwemo maafisa polisi 8 na kuzua mijadala mizito ya kitaifa juu ya ubaguzi wa rangi na polisi.
Wiki moja kabla ya kutokea kwa mauaji haya, askari polisi mweusi, Montrell aliandika hisia zake katika ukurasa wa facebook juu ya haya yanayoendelea sasa na kuelezea masikitiko yake huku akidai kuchoshwa na matukio hayo na kuwa yeyote yule atakayekutana naye na kuhitaji kumbatio au sala atakuwa tayari kufanya hivyo.