Tarehe July 23, 2016
Chama Cha Mapinduzi leo kinatarajia kumpata Mwenyekiti mpya wa Taifa, Rais John Magufuli, katika Mkutano Mkuu wa chama hicho.
Aidha, Tayari vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, vimeshapitisha kwa kauli moja jina la Rais Magufuli kugombea uenyekiti wa Taifa wa chama hicho.
Kwa mujibu wa msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka alisema kikao hicho baada ya kupokea jina la Rais Magufuli kutoka Kamati Kuu, kimeridhia lipelekwe katika Mkutano Mkuu.
“NEC kwa kauli moja imepokea pendekezo la Kamati Kuu na kutafakari na kupitisha jina la Rais John Magufuli, kugombea uenyekiti wa CCM na kesho (leo), jina hilo litawasilishwa kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM ili kuthibitishwa kwa kura za ‘Ndiyo”.
Katiba ya chama hicho ya mwaka 1997, inaeleza kuwa wakati wa uchaguzi unapofika, kazi mojawapo ya Nec ni kuteua jina la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM na kupendekeza kwa Mkutano Mkuu wa Taifa.
Katiba hiyo inasema pia kuwa unapofika wakati wa uchaguzi, kazi mojawapo ya Mkutano Mkuu wa Taifa ni kumchagua Mwenyekiti wa CCM.
Sendeka alifafanua kuwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM, ili mtu aliyependekezwa kwa nafasi ya mwenyekiti wa CCM aweze kuchaguliwa, inabidi apate zaidi ya nusu ya kura za wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa Taifa.
Alisema kwa kuwa vikao vya juu vya Kamati Kuu na NEC ndivyo vilivyompendekeza Rais Magufuli kwenye nafasi ya uenyekiti na kwa kuwa yeye mwenyewe binafsi hakuomba, wala kujaza fomu ya nafasi hiyo, basi kazi ya kumpigia kampeni itafanywa na chama chenyewe.
“Yeye hakuomba wala kujaza fomu, bali amependekezwa na NEC hivyo chama kitamsemea. Kitapita kwa wajumbe mbalimbali na kumuombea kura,” alisema.
Sendeka alisema kwenye ukumbi wa mikutano, wajumbe wawili wa NEC ndiyo watakaomwelezea na kumuombea kura kwa wajumbe ukumbini.
Kwa upande wa Mwenyekiti anayemaliza muda wake Dkt.Jakaya Kikwete alisema kumekuwa na maneno eti CCM itaishia mwaka 2020,lakini alisitiza kuwa CCM haitang’oka ng’o
Naye Katibu mkuu Abdulrahman Kinana alisema idadi ya wajumbe wa NEC waliotakiwa kuhudhuria kikao hicho ni 374, waliohudhuria ni 365 sawa na asilimia 97.5, hivyo akidi imetimia.
Fuatilia kila kinachojiri katika mkutano huo hapa hapa Hivisasa.co.tz pamoja na Sasa Tv.