Seneta John McCain apatikana na saratani ya ubongo
Seneta wa chama cha Republican John McCain amepatikana na saratani ya ubongo na anatafuta matibabu kulingana na duru za offisi yake.
Matibabu hayo huenda yakashirikisha matumizi ya dawa ama mionzi kulingana na daktari wake.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 80 yuko katika hali nzuri akiendelea kupata afueni nyumbani.
Uvumbe huo ulipatikana wakati wa upasuaji wa kuondoa damu ilioganda juu ya jicho lake la kushoto.
McCain ambaye alikuwa mwanajeshi aliyepigana vita nchini Vietnam pia alitumikia miaka mitano jela.
Seneta huyo aliyehudumu kwa mihula sita na kuwa mgombea wa urais wa chama cha Republican 2008 alifanyiwa upasuaji katika hospitali ya Phoenix katika jimbo la Arizona siku ya Ijumaa.
Uchunguzi wa tishu ulibaini kwamba uvimbe wa ubongo unaojulikana kama glioblastoma ulisababisha damu hiyo kuganda kulingana na taarifa ya kliniki hiyo ya Mayo.
Madaktari wa Seneta huyo wanasema kuwa anaendelea kupona kutoka kwa upasuaji huo na afya yake iko shwari, iliongezea.
Matibabu yake yatashirikisha utumiaji wa dawa na mionzi.
Glioblastoma ni uvimbe mbaya wa ubongo na huongezeka kutokana na umri wa mtu ukiwaathiri wanaume wengi zaidi ya wanawake.
Bwana McCain ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya sineti kuhusu hudumu za jeshi alikuwa katika hali nzuri huku akiendelea kupona nyumbani na familia yake, afisi yake ilisema.