Waziri Makamba Avunja Baraza La Mazingira NEMC
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Mhe. January Makamba leo ameivunja Bodi ya Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kutokana na tuhuma mbalimbali.
Makamba amesema kuwa sababu za mabadiliko hayo katika Bodi ya NEMC ni pamoja na ucheleweshaji wa vibali vya ukaguzi wa mazingira, tuhuma za rushwa katika usimamizi na matumizi ya lugha mbovu.
Amesema watendaji wa NEMC wamekuwa wakisaidia watu wenye maslahi nao na hata pale walipotakiwa kueleza namna wanavyofanya kazi hawakufanya hivyo.
“Kutokana na mapungufu makubwa ndani ya NEMC, tumeamua kuivunja bodi hii kuanzia leo na viongozi wengine tutawatangaza leo huku baadhi ya watendaji wa NEMC tumewasimamisha kazi ili ufanywe uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili kabla ya kuchukua hatua ,” amesema. .
Ameongeza kuwa kuanzia sasa muwekezaji atakayekamilisha kutoa taarifa ya ujenzi wa kiwanda, ruhusa ya ujenzi itatoka ndani ya siku tatu tu na kwamba wawekezaji wanaokwenda NEMC wanatakiwa kuanzia kwa washauri elekezi ili kuondoa uhusiano wao na watu wa Baraza la NEMC.
Aidha, Makamba amesema kuwa watendaji wote waliochukulia hatua leo ni baada ya uchunguzi wa awali kutosheleza kuwachukulia hatua stahiki, huku hatua nyingine zikifuata baadae.