Thursday, 20 July 2017

Majaliwa: Tutawashughulikia Wanaotoa Kauli Za Kichochezi

majaliwasafii-1

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

IMG-20170426-WA0006

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itawashughulikia watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi nchini bila ya kujali nyadhifa zao na kuwataka wananchi kuwa makini na kujiepusha kutoa matamshi ambayo yataathiri mfumo wa maisha kwa wananchi wengine.

Majaliwa amesema hayo wakati wa ibada ya mazishi ya mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Linnah Mwakyembe yaliyofanyika Wilayani Kyela.

Amesema Serikali haitavumilia kuona baadhi ya watu wakitoa matamshi ambayo hayana tija kwa jamii na badala yake yanalenga kuwavuruga wananchi na kuchochea migogoro.

“Tutashughulika na watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi, popote walipo bila ya kujali uwezo wao, vyeo vyao au mamlaka walizonazo,” amesema Majaliwa.

Aidha, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wake na kudai kuwa Serikali inawategemea sana na iko pamoja nao.

Waziri Mkuu pia amewaomba wananchi wote kushirikiana kwa pamoja katika kumuombea Dkt. Mwakyembe na familia yake ili Mwenyezi Mungu aweze kuwafariji katika kipindi hiki kigumu.

clouds stream