Rais Salva Kiir augua ghafla, mkutano wasimama
Mkutano wa viongozi wa kikanda ulioandaliwa kujadili mgogoro wa mwaka mmoja unaondelea nchini Sudan Kusini, umecheleweshwa baada ya Rais Salva Kiir kuugua na kukimbizwa hospitalini mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Afisa mmoja wa shirika la IGAD, ambalo linafanya juhudi za kuwakutanisha viongozi wa Sudan Kusini kwa lengo la kumaliza vita, amesema kwamba Rais Kiir, alianza kuvuja damu kutoka puani
Kabla ya kuugua, hapo jana Kiir alifanya mazungumzo na kiongozi wa waasi Riek Machar ambapo alimtaka kupuuzilia mbali maswala yanayochochea mgogoro huo ili kumaliza mgogoro huo ambao umedumu mwaka mmmoja
Viongozi wa kikanda, wanakutana baadaye leo, kushinikiza pande zote kufikia makubaliano ili kumaliza vita. Swala kuu kwenye ajenda, ni kusuluhisha maswala yanayoleta kizungumkuti kuhusu serikali ya muungano kama moja ya suluhu la kupatikana amani.
Pande zote zinazozozana zimekosa kufikia makubaliano kuhusu wadhifa wa waziri mkuu na ikiwa anapaswa kuwa na mamlaka makuu au la.
Maelfu ya watu wamefariki na wengine zaidi ya milioni moja kuachwa bila makao tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka nchini humo Disemba mwaka 2013.