Thursday, 29 January 2015

Prof. Lipumba alivuruga Bunge, vikao vyaahirishwa

Prof. Lipumba alivuruga Bunge, vikao vyaahirishwa

Prof Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF akisubiri hakimu katika Mahakama ya Kisutu Jijini Dar es Salaam siku ya Jumatatu tarehe 28 Januari 2015
Prof Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF akisubiri hakimu katika Mahakama ya Kisutu Jijini Dar es Salaam siku ya Jumatatu tarehe 28 Januari 2015
Kikao cha Bunge la Tanzania leo kimevurugika kutokana na vurugu za baadhi ya wabunge waliokuwa wakibishana kuhusu suala la kiongozi wa chama cha upinzani cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kushambuliwa na polisi Jumanne kwa madai kuwa alihusika katika maandamano kinyume cha sheria.
Aidha, hoja iliamshwa na mbunge ambaye pia ni kiongozi wa upinzani aliyetaka suala hilo lijadiliwe kwa dharura. Hayo yametokea huku Profesa Lipumba akifikishwa mahakamani kusomewa mashtaka ya jinai.
Chanzo cha kikao hicho  kuvurugika  ni pale aliposimama James Mbatia mbunge wa kuteuliwa kutaka suala la polisi kumshambulia na kumdhalilisha Profesa Ibrahim Lipumba, kiongozi wa chama cha CUF lijadiliwe kwa dharura bungeni humo.
Licha ya jitahada za Spika Makinda kueleza kuwa suala hilo litajadiliwa kesho, kwa kuwa serikali inahitaji muda wa kuwasilisha majibu, mambo yakavurugika.
Huku wabunge wakiwa wamesimama wima wakishinikiza hoja hiyo ijadiliwe, Spika Makinda aliendelea na msimamo wake wa kutaka hoja ijadiliwe Alhamisi baada ya serikali kuwasilisha majibu, hapo ndipo mkorogano ulipozidi na kuleta kutoelewana kati ya wabunge wa upinzani na Spika.
Spika Makinda alilazimika kuahirisha kikao hicho mpaka jioni baada ya hali kuwa ngumu, na hata jioni likaahirishwa tena mpaka kesho, Alhamisi.
Kiongozi huyo wa upinzani inadaiwa alifika eneo ambako maandamano yaliyopangwa kufanyika Jumanne yalikuwa yamepigwa marufuku, ingawa uongozi wa chama cha CUF unadai Profesa Lipumba alikusudia kuwashawishi wafuasi wake watawanyike kutii amri ya polisi ndipo akashambuliwa.
Wakati huo huo Profesa Lipumba amefikishwa mahakamani mjini Dar Es Salaam ambako amesomewa mashtaka ya kufanya maandamano bila kuwa na kibali.
Katika hatua nyingine  Profesa Lipumba alikimbizwa hospitalini baada ya afya yake kudhoofika, ikidaiwa ni sababu ya ghasia aliyoipata  jana kutoka jeshi la Polisi.
Hata hivyo alirejeshwa mahakamani baada ya kupata nafuu, na kesi yake imeahirishwa na itatajwa tena mahakamani tarehe 26 Februari 2015. Ameachiwa kwa dhamana ya watu wawili kwa kiasi cha shilingi milioni mbili kila mmoja.

clouds stream