MNARA WA MLINZI JANUARI 2015
HABARI KUU | SERIKALI ISIYO NA UFISADI
Madhara ya Ufisadi Katika Serikali
Ufisadi katika serikali umefafanuliwa
kuwa matumizi mabaya ya mamlaka ili kujinufaisha kibinafsi. Ufisadi
ulianza zamani. Kwa mfano katika Biblia, kuna sheria iliyowakataza watu
kula rushwa walipokuwa wakishughulikia kesi, kuonyesha kwamba zoea hilo
lilikuwepo zaidi ya miaka 3,500 iliyopita. (Kutoka 23:8)
Bila shaka, ufisadi unahusisha mambo mengi, si kula rushwa tu. Nyakati
nyingine maofisa wa umma huiba mali, hukubali kupokea huduma ambazo
hawastahili, au hata kuiba pesa. Hata wakati mwingine wao hutumia vibaya
vyeo vyao kuwanufaisha marafiki na pia watu wao wa ukoo.
Ingawa ufisadi unaweza kutendeka
katika shirika lolote lile la kibinadamu, inaonekana kwamba ufisadi
katika serikali umeenea zaidi. Ripoti ya mwaka wa 2013 ya Kipimo cha
Ulimwenguni Pote cha Ufisadi (Global Corruption Barometer)
iliyochapishwa na shirika la Transparency International, ilisema kwamba
ulimwenguni pote watu huviona vyama vya kisiasa, polisi, maofisa wa
umma, bunge, na mahakama kuwa taasisi zenye ufisadi mwingi zaidi. Acheni
tuchunguze ripoti kadhaa zinazozungumzia tatizo hilo.
- AFRIKA: Mwaka wa 2013, maofisa wapatao 22,000 wa umma nchini Afrika Kusini walishtakiwa mahakamani kwa sababu ya kujihusisha na ufisadi.
- AMERIKA KUSINI: Mwaka wa 2012, nchini Brazili, watu 25 walipatikana na hatia ya kutumia pesa za umma kuwashawishi wapiga kura wawaunge mkono. Miongoni mwa watu hao alikuwa waziri mkuu wa zamani, mtu wa pili mwenye cheo kikubwa nchini humo.
- ASIA: Mwaka wa 1995, watu 502 walifia ndani ya duka moja kubwa jijini Seoul, nchini Korea Kusini. Wachunguzi waligundua kwamba wajenzi waliojenga jengo hilo walijenga kwa saruji ya hali ya chini na walipuuza viwango vya usalama. Walifanya hivyo kwa kuwa maofisa wa jiji walikuwa tayari wamehongwa.
- ULAYA: Cecilia Malmström, Kamishna wa Mambo ya Ndani wa Tume ya Ulaya anasema, “Inastaajabisha sana kuona jinsi tatizo hilo [ufisadi] lilivyoenea Ulaya. Viongozi wa kisiasa wameshindwa kulikomesha.”
Si rahisi hata kidogo kwa wanadamu
kukomesha ufisadi katika serikali. Profesa Susan Rose-Ackerman, mtaalamu
wa kupambana na janga la ufisadi aliandika kwamba ili mabadiliko
yapatikane serikali inapaswa izingatie “kufanya mabadiliko makubwa
kuhusu utenda-kazi wake.” Ingawa huenda likaonekana kuwa jambo
lisilowezekana kupambana na ufisadi, Biblia inatuhakikishia kwamba kuna
mabadiliko makubwa yanayokuja, na hakika yatatimia.