Majanga yaikumba Tunduru, Mvua yaezua nyumba 51
Wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, hali sio shwari katika kijiji cha Sisi kwa Sisi tarafa ya Mlingotini kufuatia mvua kuezua nyumba 51 za makazi ya wananchi. Mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali imeharibu zaidi ya nyumba 51, wananchi wa kaya zaidi ya 25 wakikosa kabisa sehemu ya kuishi.
Akizungumzia tukio hilo mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho amesema tukio hilo la mvua kubwa kunyesha ikiambatana na upepo mkali limetokea Januari 27 mwaka huu majira ya kuanzia saa nane mpaka saa kumi mchana.
Ameongeza kuwa baraza la ulinzi na usalama la wilaya hiyo limejielekeza kwenye kijiji hicho kwa ajili ya kwenda kujionea hali halisi ilivyo ambayo ameielezea kuwa ni mbaya kwa sababu mbali ya nyumba hizo kuezuliwa, zilizo nyingi zimedondoka kwa sababu ya upepo mkali ulioambatana na mvua hiyo.
Kati ya nyumba hizo 51 zipo nyumba zilizokuwa zimeezekwa bati ikiwemo ofisi ya kijiji pamoja na ghala la mazao ya chakula huku nyumba mbili zilizoezekwa kwa nyasi nazo zimeezuliwa na kudondoka.
Katika hatua nyingine amewaomba wananchi kuzisaidia kaya zilizoathiriwa huku serikali ikiendelea kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi hao. Hata hivyo amesema kuwa hadi sasa hasara iliyopatikana bado haijafahamika.