Huyu ndio Mwanadada aliyevuliwa nguo na Maofisa wa CAF wakidai ni Mwanaume
Nyota tegemezi wa timu ya Taifa ya wanawake ya mpira wa miguu ya Equatorial Guinea, Genoveva Anonma, kwa taklibani miaka minne sasa amekuwa akiishi na dukuduku moyoni huku akijawa na hofu kufatia kitendo ambacho kinaonekana ni cha unyanyasaji wa kijinsia alichofanyiwa na maofisa wa Shirikisho la mpira wa miguu Afrika CAF wakidai kuwa yeye ni mwaume.
Genoveva ambaye anakipiga katika labu ya Turbine Potsdam nchini Ujerumani katika ligi maarufu ya Bundesliga tangu mwaka 2011. Mwaka 2008 katika michuano ya mataifa ya Afrika kwa wanawake, Shirikisho la CAF kupitia maafisa wake liliamuru mchezaji huyo akaguliwa jinsia yake kwa kuvuliwa nguo zake zote mbele ya maafisa hao na mbele ya wachezaji wenzake baada ya kuzuka uvumi kuwa anajinsia ya kiume.
Kufatia kitendo hicho Genoveva Anonma, analaani sana kwani alifanyiwa ukatili mkubwa wa kijinsia kitu ambacho kilimfanya nguvu kumuishia hata alipokuwa uwanjani alicheza ka kutojiamini kama awali.
“Nilifedheheka mno,hata ari ya mchezo ilishuka na nilikuwa nalia mno,ilikuwa ni udhalilishaji tosha,lakini ilinilazimu kutekeleza amri” Amesema Nyota huyo ambaye kwa wananchi wa Equatorial Guinea, huwaambii kitu kwenye timu yao ya Taifa ya wanawake.
Genoveva Anonma ambaye alilelewa na mama yake pekee baada ya baba yake kuwakimbia na kuishi na mwanamke mwingine, alijikuta akitengwa na wasichana wenzake enzi za udogo kufatia yeye kupenda kucheza mpira wa miguu kitu ambacho wenzake walikuwa wakimchukulia tofauti sana, lakini yeye hakuona ishu sana akaamua kuwa beneti na watoto wenzake wa kiume wakisakata kabumbu.
Alijikuta akiingia kwenye mgogoro mzito na mama yake baada ya kumtaka aachane na soka na akili yake aihamishie shuleni ambapo mzazi wake huyo alitaka Genoveva Anonma asome hadi chuo kikuu ili aje kuwa mwalimu, lakini kwakuwa damu ya mpira ilikuwa imekwisha enea mwilini mwake alipuuza maneno ya mama na kuendeleza kusukuma gozi hadi mama yake huyo alipomfukuza nyumbani na kuamua kukimbilia kwa mjomba wake.
“Baba yangu alikuwa anaishi katika mji mwingine na mwanamke mwingine, na mama yangu alikuwa akipambana na mimi kila wakati niache kucheza mpira wa miguu, alikuwa akinitaka nisome hadi kufikia hatua ya digirii na niwe mwalimu ama nibobee katika masuala ya kuwasaidia watoto, Tulikuwa hatuelewani, na ndipo akaapa kuwa hataki kuniona tena nyumbani, nami nikaondoka nyumbani na kwenda kuishi na mjomba wangu, mjomba hakuwa na matatizo nami akanipeleka mjini huko nikaendelea na masomo yangu na sikuacha kucheza mpira” Amesema Nyota huyo.
Alipokuwa na umri wa miaka 16 mwaka 2003, alijiunga na timu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, na baadaye akajiunga na klabu ya Jena ya Ujerumani ilikuwa katika ligi ya Bundesliga, akiwa na timu hiyo aliwika na kuwa mfungaji bora wa Jena kwa misimu miwili mfululizo.
Mwaka 2011 aliibuka Mshindi wa michuano ya kombe la mataifa ya Afrika kwa wanawake, ambapo Nigeria, pamoja na nchi zingine ikiwemo Afrika Kusini, Ghana, waliishutumu Guinea kwakuwa na wachezaji watatu wa kiume katika timu yao wachezaji hao ni ndugu wawili Salimata na Bilguisa Simpore, na nahodha wao Anonma.
Baada ya Taarifa za watatu hao kuwa ni wanaume zilipoanza kusambaa katika mitandao ya kijamii Anonma akaamua kuvunja ukimya na kwenda mbele ya vyombo vya habari kukana shutuma hizo.
Na Anonma anadai kuwa yote hayo yanakuja kwasababu yeye ni mwepesi na mwenye kasi ya ajabu awapo mchezoni,lakini anajitambua kuwa ni mwanamke.