Sunday 8 October 2017
IGP Sirro Ataka Mjadala Kuhusiana Na Lissu Ufungwe
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro.
Mkuu wa Jeshi la Polisi chini (IGP), Simon Sirro amesema kuwa mjadala kuhusiana na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema),Mhe. Tundu Lissu kupigwa risasi ufungwe mara moja ili Jeshi lifanye kazi yake.
IGP Sirro ametoa agizo hilo akiwa ziarani Mkoani Mbeya na kudai kuwa Jeshi la Polisi ndilo lenye dhamana ya kufanya uchunguziwa tukio hilo na kulitolea ufafanuzi.
Aidha, amesema hataki malumbano na familia ya Mbunge huyo kuhusiana na namna uchunguzi wa tukio hilo unavyofanywa auutakavyofanywa.
Hivi karibuni familia ya Lissu kupitia kwa kaka wa Lissu, Alute Mughwai Lissu ilikaririwa ikitaka Serikali na Jeshi la Polisi kuruhusuwachunguzi wa kimataifa kutoka nje ya nchi kuja kuchunguza tukio hilo.
Mbali na kutaka wachunguzi kutoka nje, familia hiyo pia ilitoa rai kwa Jeshi la Polisi kutumia ubalozi wake nchini Kenya kumhojidereva wa Lissu ambaye anadaiwa yupo Jijini Nairobi akiendelea na matibabu.
Pamoja na familia hiyo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimekuwa kikitoa matamko mbalimbali kuhusiana na tukio hilo, ikiwa ni pamoja na kutaka wachunguzi kutoka nje ya nchi kufanya kazi hiyo ya upelelezi ili kujua kilichotokea.
Mhe. Lissu alishambuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasioujulikana Septemba 7, mwaka huu akiwa nyumbani kwake Area D,Mkoani Dodoma na kukimbizwa Jijini Nairobi ambapo anaendelea kupata matibabu hadi sasa.