Monday, 30 October 2017

Mbunge wa CCM Lazaro Nyalandu ajiuzulu Tanzania

Bw Nyalandu

Mbunge wa chama tawala nchini Tanzania CCM Lazaro Nyalandu amejiuzulu wadhifa wake, na kusema kwamba anataka kuhamia chama cha upinzani Chadema.

Bw Nyalandu, Aliyekuwa Waziri wa Mali Asili na Utalii wakati wa serikali ya awamu ya Tano nchini Tanzania amesema kupitia taarifa kwamba amejuzulu nyadhifa zake zote ndani ya chama cha mapinduzi CCM ikiwemo ubunge.

Nyalandu ambaye kabla ya maamuzi hayo ya kujiuzulu alikuwa Mbunge wa Singida Kaskazini amesema amechukua uamuzi huo kutokana na kutokuridhishwa na mwendo wa siasa nchini Tanzania, ukiukwaji wa haki za kibinaadamu, ongezeko la vitendo vya kidhalimu dhidi ya raia na kutokuwepo kwa mipaka baina ya mihimili ya dola - Serikali, Bunge na Mahakama.

Katika taarifa yake ya kujiuzulu aliyoiweka katika ukurasa wake wa Facebook, Nyalandu amesisitiza umuhimu wa nchi hiyo kupata katiba mpya.

"Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa, hakuna namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali," amesema.

"Nimemua kujiuzulu Kiti cha Ubunge, Jimbo la Singida Kaskazini kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi mwingine ili wananchi wapate fursa ya kuchagua itikadi wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye changamoto lukuki nchini Tanzania.

"Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo."

Nyalandu anaingia katika orodha ya mkururu wa viongozi wa juu wa CCM waliokihama chama hicho na kuhamia chama kikuu cha upinzani nchini humo Chadema tangu mwaka 2015.

clouds stream