Friday, 27 October 2017
JAHAZI LAKAMATWA LIKISAFIRISHA HEROIN YA BILIONI 5
Dawa za kulevya aina ya Heroini.
Maofisa wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) wakishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wamekamata zaidi ya kilo 100 za madawa ya kulevya aina ya Heroin zenye thamani ya Shilingi bilioni 5 zilizokuwa zikisafirishwa kwenye jahazi kutoka Unguja kwenda Dar es Salaam.
Kamishna wa Sheria wa DCEA, Edwin Kakolaki amesema hatua hiyo ilifikiwa baada ya maofisa hao kutilia shaka jahazi hilo ambalo ndani yake lilikuwa na raia kumi wa Iran na Wazanzibari wawili.
“Paketi 104 za madawa ya kulevya yanayoshukiwa kuwa ni heroin zilikamatwa katika jahazi hilo na kupelekwa kwa Mkemia Mkuuwa Serikali kwa vipimo zaidi,” amesema.
Amesema hadi jana jioni walikuwa wamefanya upekuzi kwa kusaidiana na mbwa maalum wa kunusa ili kuona kama kuna mzigo zaidi katika jahazi hilo.
Naye Kamishna Mkuu wa DCEA, Rodgers Siang’a amesema kiwango cha dawa hizo kingekuwa kikubwa zaidi kama sio kitendo cha watu hao kutupa kiasi kingine baharini baada ya kuzidiwa nguvu walipozungukwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Vyombo vya dola viko imara kupambana na usafirishaji wa dawa za kulevya na hatutaacha kuyadhibiti magenge na mitandao yao,” amesema Siang’a.
Hatahivyo, upekuzi huo haukukamilika kutokana na hali ya mvua ambapo unatarajiwa kuendelea leo huku taratibu za kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali zikikamailika, watuhumiwa hao watapelekwa mahakamani.