Monday, 30 October 2017

RAIS MAGUFULI APONGEZA MABADILIKO CUF



Daraja la Furahisha



Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaunga mkono mabadiliko yanayotokea katika Chama cha Wananchi (CUF) na kupongeza hatua hiyo.

Rais Magufuli amesema hayo leo Jijini Mwanza wakati wa ufunguzi wa daraja la Furahisha litakalotumiwa na waenda kwa miguuMkoani humo.

Akikamilisha hotuba yake na kumtambua Mbunge wa Liwaled, Mhe. Zuberi Kuchauka (CUF), Rais Magufuli amesema wanawapongeza CUF kwa mabadiliko wanayofanya na kumtaka mbunge huyo kufikisha salamu zake na pongezi nyingi kwa mabadiliko hayo.

“Tunawapongeza sana kwa mabadiliko mnayofanya na ukawafikishie salamu zetu,” amesema Rais Magufuli.

Awali mbunge huyo alipopewa nafasi ya kusema machache, alimmiminia sifa nyingi Rais Magufuli na kumuombea dua ili awe na afya njema aweze kutimiza lengo lake na kukuza viwanda na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati.

“Mhe. Rais, sisi sote tunatambua kazi nzuri unayoifanya ya kuwaletea maendeleo Watanzania na mimi napenda nikupongeze sana kwa hilo na ndiyo maana nakuombea dua uzidi kuwa na afya njema,” amesema.

Hivi karibuni CUF imekuwa katika hekaheka na migogoro isiyokwisha na kupelekea chama hicho kupasuka vipande viwili, ambapo upande mmoja unaamini katika CUF ya Mwenyekiti anayetambulika na Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof. Ibrahim Lipumba huku upande wa pili ukiwa unaamini katika CUF ijulikanayo kama CUF Maalim, ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF.

clouds stream