Gianluigi Buffon ameshinda Serie A mara kumi
Shirikisho la soka duniani Fifa limetangaza kikosi bora cha soka ya wanaume duniani mwaka 2017 ambapo kuna mabadiliko matatu kutoka kwa kikosi kilichotangazwa mwaka 2016.
Mshambuliaji wa PSG Neymar, ambaye ndiye mchezaji ghali zaidi duniani naye ameingia nafasi ya Luis Suarez katika safu ya mashambulizi.
Kikosi hicho kina wachezaji watano kutoka Real Madrid, wawili wa Barcelona, wawili wa PSG, mmoja wa Juventus na mmoja kutoka AC Milan.
Hakuna mchezaji hata mmoja wa Ligi ya Premia aliyefanikiwa kujumuishwa katika kikosi hicho.
Mkufunzi bora duniani soka ya wanaume
Zinedine Zidane amemshinda meneja wa Chelsea Antonio Conte baada ya kuongoza Real Madrid kushinda La Liga msimu uliopita kwa mara ya kwanza tangu 2012 na kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mtawalia msimu uliopita.Conte alishinda Ligi ya Premia msimu uliopita.
Massimiliano Allegri wa Juventus, ambaye aliongoza klabu yake kushinda Serie A na Coppa Italia msimu uliopita alikuwa wa tatu.
Mkufunzi bora soka ya wanaume | ||
---|---|---|
Zinedine Zidane - 46.22% | Antonio Conte - 11.62% | Massimiliano Allegri - 8.78% |
Mkufunzi bora duniani soka ya wanawake
Kocha wa Uholanzi Wiegman aliyeongoza Uholanzi kushinda Euro 2017 nyumbani kwao amechukua taji hilo.Waliwalaza Denmark kwenye fainali.Sarina Wiegman akipokea taji lake
Mkufunzi bora wa soka ya wanawake | ||
---|---|---|
Sarina Wiegman - 36.24% | Nils Nielsen - 12.64% | Gerard Precheur - 9.37% |
Kipa bora zaidi
Mshindi wa Kombe la Dunia na mshindi wa Serie A mara 10 Gianluigi Buffon ndiye mshindi wa tuzo ya mlindalango bora duniani mwaka huu.Aliwasaidia Juventus kushinda taji la ligi mara ya sita mtawalia msimu uliopita.
Aidha, alicheza dakika 600 Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya bila kufungwa.
Buffon, 39, amewashinda kipa Keylor Navas, wa Real Madrid na Manuel Neuer wa Bayern Munich.
"Ni heshima kubwa sana kwangu kupokea tuzo hii katika umri wangu huu," alisema Buffon.