Thursday 12 October 2017
SHEIKH PONDA AELEZA JINSI ALIVYOPEWA MATUMAINI NA LISSU
Sheikh Ponda.
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda amesema ameguswa na hisia za Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Mhe. Tundu Lissu pale alipokwenda kumtembelea hospitalini Jijini Nairobi alipolazwa akiendelea kupatiwa matibabu baada ya kushambuliwa na kupigwa risasi.
Ponda amesema hayo leo Jumatano mbele ya waandishi wa habari akizungumzia safari yake ya Nairobi nchini Kenya alikokwendakumjulia hali Lissu hivi karibuni na kudai kuwa amemueleza kuwa atarudi katika harakati hivi karibuni na ataanzia alipoishia.
Amesema madhumuni ya safari yake yalikuwa kumjulia hali Lissu, kumwombea dua, kumjengea matumaini ya afya na kujenga mazingira mapana yanayotosha kulizungumza jambo lililomfika kwani hata yeye mwaka 2013 alipigwa risasi, lakini mwaka huu amepigwa Lissu na kuomba wananchi wajitokeze kukemea matukio kama hayo.
“Tulipokuwa tunabadilisha mawazo, niliguswa na hisia kubwa, badala ya mimi kumpa matumaini yeye ndiye alinipa matumaini,” amesema Ponda.
Aidha, amesema Mhe. Lissu amehimiza mshikamano kuonesha kuwa ana matumaini na Watanzania kwa harakati wanazozifanya.
Awali, Jeshi la Polisi lilifika katika mkutano huo ulioandaliwa na Sheikh Issa Ponda na kuwakamata baadhi ya waandishi wa habari.
Lissu alijeruhiwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka huu akiwa nyumbani kwake Area D Mjini Dodoma majira ya mchana akiwa anatoka Bungeni.