Wednesday 18 October 2017

LISSU KUTIBIWA AWAMU YA TATU NJE YA NAIROBI ,KAMERA CCTV YAIBUA MAMBO




Tundu Lissu.



Mwenyekiti wa Chadema, Mhe. Freeman Mbowe amesema kuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu
anaendelea vizuri sasa na hatumii tena mirija kwa ajili ya kula chakula bali anakula mwenyewe na anakula chakula anachokitaka
na kwa mara ya kwanza ameweza kutoka Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), na kuliona jua tangu afikishwe hospitalini.
Mbowe amesema hayo leo Jijini Dar es Salaam alipokutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa taarifa za maendeleo ya
Mhe. Lissu na kudai kuwa licha ya maendeleo hayo mazuri, muda sio mrefu Mhe. Lissu ataanza awamu ya tatu ya matibabu.
Amesema Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), amefanyiwa upasuaji mara 17 na kwamba ni
maajabu ya Mungu kwamba Kiongozi huyo ni mzima na anaendelea kupumua vizuri baada ya misukosuko yote.
“Tunatarajia baada ya muda kidogo ataanza matibabu ya awamu ya tatu ambayo hayatakuwa Nairobi tena,” amesema Mhe.Mbowe.
Mbowe ameongeza kuwa katika awamu ya tatu ya matibabu, wataiachia familia nafasi ya kufanya maamuzi na kuweza kusaidia
pale watakapohitajika kusaidia.
Aidha, Mhe. Mbowe amehoji ni kwanini kamera za ulinzi za CCTV zilizokuwepo eneo la tukio Mjini Dodoma wakati Lissu
aliposhambuliwa kwa kupigwa risasi zimeondolewa.
“Lissu ameshambuliwa lakini ilichukua masaa mawili kwa polisi kufika kwenye eneo la tukio, kwanini tusiingie hofu?, pia Mh.Lissu
ni jirani wa Waziri, tuna taarifa kuwa ile CCTV Camerailiyokuwepo eneo la tukio imeondolewa, je imeondolewa na nani?,”amehoji Mbowe.
Mhe. Lissu alishambuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana, Septemba 7, mwaka huu akiwa kwenye gari lake, nyumbanikwake Area D, Mkoani Dodoma, majira ya mchana akiwa anatoka bungeni.
Tangu wakati huo hakuna mtu yeyote Yule aliyetiwa nguvuni kuhusiana na tukio hilo la kinyama huku Jeshi la Polisi likiendelea nauchunguzi kubaini wahusika wa tukio hilo.
Wakati uchunguzi ukiendelea, Mhe. Lissu amekuwa kitandani alipolazwa katika Hospitali ya Jijini Nairobi, Kenya akiendelea na
matibabu.

clouds stream