Monday, 16 October 2017
Nkamia Aibua Mapya Hoja Binafsi Ukomo Wa Bunge, Nape Afunguka
Juma Nkamia, Mbunge wa Chemba (CCM).
Wakati kukiwa na taarifa zisizo rasmi zinazozagaa katika mitandao ya kijamii tangu jana, Oktoba 14, 2017 zikidai kuwa Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia amelazimika kuondoa kwa muda hoja yake binafsi ya ukomo wa bunge ambayo alikusudia kuiwasilisha katika bunge lijalo baada ya mashauriano na maelekezo ya viongozi wa juu wa CCM, Mbunge mwenzake wa Jimbo la Mtama (CCM), Mhe. Nape Nnauye amepigilia msumari kauli iliyotolewa na Spika wa zamani wa Bunge , Pius Msekwa.
Mhe.Nape amesema misimamo hiyo ndiyo misimamo ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwalimu Julius Nyerere.
Mhe. Nnauye ameweka kipande cha video inayomuonesha Mzee Pius Msekwa akielezea juu ya ukomo wa kiongozi madarakani na kusema chama hicho kilishafikiria miaka ya nyuma kuongeza miaka kutoka 10 na kuendelea lakini waliona miaka kumi inatosha kwa mtu kuongoza na kusisitiza ikiwa miaka 15 ikatokea mkapata kiongozi mbaya miaka hiyo itakuwa ni mingi sana.
“Miaka 15 mkipata kiongozi mbaya ni mingi sana, nashauri ibaki miaka 10 kama kiongozi ni mbaya angalau tumvumilie kwa miaka 10 tu halafu basi ndivyo hoja ya miaka 10 ilivyopita si kama hiyo mingine hatukufikiri ilifikiriwa ndiyo maana naposikia kuna Mbunge mmoja anataka kupendekeza twende kwenye miaka saba kwa vipindi viwili ninataka kumjulisha kwamba hili si wazo jipya
tulishafikiri na lilikataliwa kwa hiyo mimi na imani CCM itaendelea kulikataa hilo, tutabaki kwenye miaka mitano tu mara mbili basi,” amenukuliwa akisema Msekwa.
Kufuatia kauli hiyo ndipo Nape Nnauye akashindilia na kusema kuwa hicho ndicho Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha Mwalimu JuliusNyerere anachokijua yeye.
Siku za karibuni Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia alidai anataka kupeleka hoja bungeni kuongeza muda wa utawala hadi
miaka 7 badala ya miaka mitano ya sasa.
Hatahivyo, Nkamia amesema kuwa kesho ataweka hadharani taarifa yake kuhusiana na minong’ono inayoendelea nchini kuwa ameondoa hoja yake.
“Nitazungumza na waandishi wa habari Jumatatu nitaeleza ukweli,” amesema Nkamia alipoulizwa kuhusiana na uvumi huo wakuondoa hoja yake.