Monday 19 September 2016

Wake Wa Waliouawa Kesi Ya Zombe Wamlilia JPM.

Tarehe September 19, 2016
Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kinondoni, SP Christopher Bageni akisindikizwa kupanda gari la askari baada ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kinondoni, SP Christopher Bageni akisindikizwa kupanda gari la askari baada ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Familia ya mmoja wa marehemu katika mauaji wafanyabiashara wa madini, Martha Martine amemuomba Rais John Magufuli kuwasaidia yatima walioachwa na marehemu.

Martha Martine ambaye alikuwa mke wa marehemu Mathias Lunkombe ameyasema hayo baada ya Mahakama ya Rufaa kutoa hukumu dhidi ya vigog wa polisi na kudai kuwa hawezi kupingana nayo, badala yake ameeleza namna kifo cha mumewe kilivyoiathiri familia, hususan watoto wawili alioachiwa.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa juzi, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Kinondoni, Christopher Bageni alihukumiwa kunyongwa hadi kufa huku Abdallah Zombe na wenzake wawili wakiachiwa huru.

Hukumu hiyo ilitolewa baada ya rufani ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye hakuridhishwa na hukumu ya Mahakama Kuu ambayo iliwaachia huru washtakiwa hao.

Bageni alikuwa ni miongoni mwa washtakiwa kwenye kesi hiyo iliyokuwa inawakabili askari polisi tisa akiwamo Zombe ambaye alikuwa Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam.

Wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, ndugu yake Eprahim Chigumbi na Mathias Lunkombe na dereva teksi, Juma Ndugu waliuawa Januari 14, 2006 kwenye Msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, Dar es Salaam.

Kutokana na hukumu hiyo, Martha amesema kwa sasa anaishi maisha magumu kwa kuwa anatumia fedha nyingi kuwasomesha watoto wake Grace anayesoma kidato cha nne na Fulmes anayesoma kidato cha pili.

Amesema Serikali ilimuahidi kumsaidia kutunza watoto lakini hakuna msaada wowote alioupata kutoka serikalini wala kwa kiongozi yeyote.

Kutokana na hali hiyo, Martha amemuomba Rais Magufuli kuwasaidia watoto hao kupata elimu na mahitaji mengine muhimu ili waweze kuja kujitegemea kimaisha.

Mdogo wa marehemu Protas, Mathias Lunkombe amesema tangu kaka yake alipofariki amekuwa akihudumia familia mbili, ya kwake na ya marehemu kaka yake.

Kuhusu hukumu iliyotolewa, amesema haki imetendeka kwa kumhukumu Bageni kunyongwa hadi kufa japokuwa hakuna hukumu ambayo ingeweza kupoza au kuondoa machungu waliyonayo kwa ndugu yao aliyeuawa.

“Pamoja na kumuua kaka yangu lakini kifo chake ni cha kumdhalilisha kwa sababu walimsingizia kuwa ni jambazi ilhali ni mfanyabiashara wa madini,” amesema.

Wakati familia ya Lunkombe ikisema hayo, Mke wa Bageni, Stella Saria amekataa kuzungumzia hukumu ya kifo iliyotolewa kwa mumewe.

“Mimi ni askari, nipo chini ya Kamishina (wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon) Sirro, siwezi kuongea na waandishi wa habari siruhusiwi kuongea chochote,” amesema.

Ameongeza kuwa Kijeshi tuna miiko ya kazi, kama mume wangu amepata matatizo hayo ni mambo ya kawaida, mimi nina viongozi wangu wa kazi, nilivyofundishwa kama ni kitu cha familia yangu, Christopher alikuwa ofisa wa polisi watajibu viongozi wake wapo.

“Mimi nina amani ya kutosha, ni Mkristo nimempokea Yesu, tatizo haliwezi kunitokea nikadharau miiko ya kazi. Mimi ni kiongozi askari, naelewa miiko ya kazi lazima niiheshimu, samahani,” amesema.

clouds stream