Thursday, 2 June 2016

AHADI YA MILIONI 50 KILA KIJIJI YATENGEWA PESA ‘KIDUCHU’

Ahadi ya Rais John Magufuli ya kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji kwa ajili ya kusaidia vikundi vya wajasiriamali wanawake na vijana, imeanza kutekelezwa baada ya Wizara ya Fedha na Mipango kutenga Sh bilioni 59.6 katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2016/17.

Wakati akiomba kura kwa Watanzania kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, Dk Magufuli aliahidi kuwa katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), atatoa kwa kila kijiji Sh milioni 50 kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana.pesa

Katika Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango iliyowasilishwa jana bungeni na Waziri Dk Phillip Mpango, inaomba kuidhinishiwa Sh trilioni 9.5 ambazo miongoni mwa hizo, zimo Sh bilioni 59.5 za kutekeleza ahadi ya Dk Magufuli.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti katika taarifa yake iliyosomwa na Makamu Mwenyekiti wake, Mbunge wa Kalambo, Josephat Kandege (CCM) ndiyo iliyoibua hoja hiyo. Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo, iliyonukuu kitabu cha mafungu ya fedha, serikali imetenga Sh bilioni 59.5 kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hiyo ya kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji na kila mtaa nchi nzima.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa, ilipofanya tathmini ya vijiji na mitaa ya Tanzania Bara tu, ikakuta kuna vijiji na mitaa 19,600, ambayo ili kila kimoja kipate hizo fedha, kunahitajika Sh bilioni 980.

Kwa uchambuzi uliofanyika, fedha zilizotengwa katika bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hiyo kwa mwaka ujao wa fedha ni asilimia sita tu ya mahitaji, ambayo inatosha kutekeleza ahadi hiyo kwa ajili ya vijiji 1,190 tu, kati ya vijiji 19,600 vya Tanzania Bara.

clouds stream