Tarehe June 30, 2016
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kutekeleza agizo la Rais Dkt John Magufuli la kujenga Ofisi Kuu ya Tumemjini Dodoma baada ya jana kuoneshwa kiwanja katika eneo la Iyumbu katika Manispaa ya Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Damian Lubuva, amesema katika uchaguzi zijazo wataanza shughuli za usimamizi wakiwa Dodoma.
“Katika Uchaguzi Mkuu ujao, wapambe wa wagombea watakaa nje ya viwanja hivi wakiwasubiri watu wao wachukue fomu, huu ni mwanzo wa safari yetu ya kuhamia rasmi mjini Dodoma,” alisema Jaji Lubuva akionesha kiwanja hicho ambacho kimenunuliwa kutoka Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA).
Akizungumza baada ya kukagua eneo la ekari 10 litakalotumika kujenga ofisi hizo, Lubuva alisema huo ni mwanzo wa safari ya kuhamia Dodoma na kwamba tume ilikuwa na lengo la kuwa na jengo la kutosheleza mahitaji kwa muda mrefu kwani sasa ofisi ya tume hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam ina ofisi tatu maeneo matatu tofauti.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Kailima Ramadhani alisema eneo hilo lina miundombinu yote na wameanza mazungumzo la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ili ifikapo Oktoba ujenzi uanze na baada ya mwaka mmoja tume iwe na jengo lake.