Monday, 6 June 2016

Naibu Spika Kujadiliwa Leo Bungeni

Naibu Spika Kujadiliwa Leo Bungeni

Tarehe June 6, 2016Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson.
Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson.
Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson.
Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashillilah leo ataeleza kinachoendelea kuhusu kusudio la Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutaka kumwondoa madarakani Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.
Kambi hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe katika migomo yake dhidi ya vikao vinavyoongozwa na Dkt. Ackson, iliwasilisha kusudio hilo kwa Ofisi ya Spika wa Bunge wiki iliyopita kwa maelezo kuwa haina imani naye.
Kwa mujibu wa Dkt. Kashillilah, ataeleza kinachoendelea leo baada ya kumaliza kupitia taratibu zote na kujiridhisha kuhusu kila hatua inayopaswa kufuatwa kuhusu suala la aina hiyo.
“Nitaeleza kinachoendelea leo baada ya kujiridhisha kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa kuhusu suala hilo,” amesema.
Katika kusudio hilo lililowasilishwa na Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya, Kambi hiyo ya Upinzani ilieleza mambo sita yaliyoisukuma kuona kuwa Dkt. Tulia hafai kuendelea kushika kiti cha Naibu Spika.
Mambo hayo ni upendeleo kwa wabunge wa CCM, kusimamia maslahi ya Serikali badala ya umma, kutokuwa mwanasiasa, jambo linalomfanya akose uzoefu wa kuendesha vikao vya Bunge, ubabe, unyanyasaji kwa wabunge wa upinzani na kusimamia fedha za Mfuko wa Bunge zirudishwe kwa Rais.
Millya alisema walipeleka kusudio hilo kwa Ofisi ya Spika kwa kuzingatia ibara ya 85(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayozungumzia hatua za kuchukua ili kumwondoa madarakani Naibu Spika.
Hili linakuja wakati wabunge wa upinzani wakiwa wameazimia kuzunguka nchi nzima kuongea na Watanzania na kuwaeleza baadhi ya mambo yanavyokwenda nchini mojawapo ikiwemo suala la kutokuwa na imani na Naibu Spika huyo.

clouds stream