Tarehe June 25, 2016
Mwenyekiti wa TLP taifa Dkt. Augustine Lyatonga Mrema amesema kuwa nchi hii haiwezekani kila siku ikawa ni maandamano kwani wananchi wanatakiwa wafanye kazi.
Mrema alisema hayo alipokuwa akizungumzia kuhusu kauli ya Rais ya kuzuia mikutano ya kisiasa hadi mwaka 2020 kama haitaviathiri vyama kikiwemo chama anachokiongoza cha TLP.
Mrema alisema sababu ya kufutwa kwa mikutano hiyo imechangiwa na wapinzani wenyewe kufuatia kususia vikao vya Bunge na kuitisha mikutano ya kisiasa nchi nzima ikiwa hivisasa wananchi wanatakiwa kufanya kazi.
”Kwa maoni yangu binafsi hii imetokana na tabia yetu sisi wapinzani kugomea kila kitu hata mambo ambayo yana maslahi kwa taifa, kwa mfano ukiangalia wakati Rais Dkt. John Magufuli anazindua bunge la bajeti wapinzani walimgomea na kutoka nje, hapa walianza kumhukumu kabla hajaanza kazi”- Amesema Mrema.
Kuhusu chama chake kutofanya siasa Mrema amesema yeye hana maandamano ya kila mara hivyo anaamini atakuwa na mikutano halali muda ukifika lakini kwa sasa wananchi wafanye kazi kwanza.