Tarehe June 16, 2016
Serikali inakusudia kutunga sheria ya kupiga marufuku ajira za wasichana wa kazi wenye umri chini ya miaka 18 kabla ya mwisho wa mwaka 2016.
Hatua hiyo inaelezwa inakusudia kuinua hadhi ya kazi na ajira za wasichana wa kazi nchini, kwani muda wa kurasimisha ajira hizo umefikia wakati wake.
Hayo Mjini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu wakati akizungumzia na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika inayoadhimishwa tarehe 16 Juni kila mwaka.
Amesema hatua hiyo inachuliiwa na Serikali kutokana na wasichana wengi wa ndani kutumikishwa kazi hiyo katika umri mdogo na kulipwa ujira mdogo.
“Tumepanga kutunga kanuni na sheria ya kupiga marufuku ajira za wasichana wa kazi wenye umri chini ya miaka 18, na ndio maana tunawachukua katika umri mdogo sana na kuwalipa ujira mdogo, hivyo ukimchukua binti wa miaka 18 utaweza kuinua hadhi ya kazi ya kazi yenyewe” amesema Waziri Ummy.
Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo, Waziri Ummy ameitaka jamii kukataa kurubuniwa kwa pesa na katika kuwafichua watu wanaofanya vitendo vya ukatili kwa watoto ikiwemo kulawiti na kuwabaka na badala yake watoe taarifa katika vyombo vya dola ili adhabu kali zichuliwe dhidi yao.
Aidha Waziri Ummy amewata wazazi nchini kujenga tabia ya kukagua maumbile ya watoto wao hususani watoto wa kike ikiwemo kuwaogesha angalau mara moja kwa mwezi, kwani kwa kufanya hivyo kutamwezesha mzazi kufahamu afya ya kimwili ya motto wake.
Kwa mujibu wa Waziri huyo amesema vitendo vya ulawiti havifanywi kwa watoto wa kike pekee bali na watoto wa kiume pia wamekuwa wahanga wa vitendo hivyo, ambapo ameitaka jamii kutowaamini ndugu au jamaa zao kulala kitanda chumba kimoja na watoto wao.
“Kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi, vitendo hivi vimekuwa vikifanyika zaidi majumbani kwa asilimia 49, ambapo asilimia 23 ni wakati wa kurudi au kwenda shule huku asilimia 15 ni wakati wakiwa shuleni, hivyo kwa takwimu hizi unaweza kuona ukubwa wa tatizo ulivyo” amesema Waziri Ummy.