Tarehe June 17, 2016
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imesema kuwa mafundi umeme 2,000 pekee ndio wenye vibali vya kufanya kazi hiyo nchini.
Imesema mafundi wengi wanaofunga umeme nyumbani na kwenye ofisi mbalimbali hawana vibali vya kufanya kazi hiyo, hivyo kuendesha shughuli hiyo kinyume cha sheria.
Mkurugenzi wa Umeme kutoka Ewura, Anastas Mbawala alisema hayo Dar es Salaam jana wakati wa semina ya kufahamu kanuni mpya za ufungaji umeme kwa makandarasi.
Amesema mafundi umeme hupewa vibali vya kazi kulingana na madaraja wanayoyapata na kuwa kanuni mpya zinataka mtu anayefanya shughuli za ufungaji umeme kuwa na leseni kwa lengo la kuhakikisha shughuli hizo zinafanywa na watu wenye taaluma stahiki, ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao.
“Sheria inataka kazi zote za ufungaji umeme ikiwa ni pamoja na upanuzi, marekebisho na matengenezo kwenye mifumo ya umeme zifanywe na fundi mwenye leseni iliyotolewa na Ewura na ni kosa kisheria kufanya shughuli za ufungaji umeme bila ya kuwa na leseni ya mamlaka hiyo,” amesema.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu atakayepatikana na hatia atatozwa faini ya Shilingi milioni tano au kifungo cha miaka mitano jela au vyote kwa pamoja.
Alieleza zaidi kuwa, kanuni mpya za ufungaji umeme zinamtaka mmiliki wa jengo kukagua mifumo ya umeme kwenye jengo lake mara kwa mara.