Tarehe June 8, 2016
Jeshi la Polisi limelazimika kuwatawanya wanachama wa Chadema kwa kutumia mabomu ya machozi waliohudhuria mkutano ulioandaliwa na chama hicho.
Mkutano huo ulipangwa kufanyika leo hii mjini kahama mtaa wa CDT huku mamia ya wananchi wakijitokeza kusikiliza mkutano huo ambapo ulikatizwa na mabomu kutoka Jeshi hilo la Polisi ambayo yalichukua takribani nusu saa.
Kufuatia mkutano huo kusitishwa Jeshi la Polisi kupitia Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Nsato Masanzya ametangaza kupiga marufuku mikutano yote ya kisiasa nchini kwa madai kuwa hali ya usalama bado haijatengemaa.
ACT-Wazalendo wanena;
Chama cha ACT Wazalendo kimelaani vikali uamuzi wa jeshi la polisi kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa uliotangazwa leo na Kamishna wa Polisi-Operesheni na Mafunzo Nsato M Msanzya-CP.
Kwa mujibu wa Ado Shaibu Katibu Itikadi, Mawasiliano na Uenezi amesema Chama cha ACT-amesema ACT- Wazalendo kinapinga vikali uamuzi wa jeshi la polisi kwa sababu hauna mashiko kwa kuwa haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ni ya kisheria kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 (kifungu cha 11(1).
“Uamuzi huu wa Jeshi la Polisi unavunja haki ya raia kutoa maoni (Ibara ya 18(a) na uhuru wa kukusanyika (Ibara ya 20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Alisema Shaibu
Amesema sababu iliyotolewa na Jeshi la Polisi kuwa mikutano hii inalenga kuchochea wananchi kutotii sheria ni mwendelezo wa visingizio vya serikali vinavyolenga kuminya uhuru wa wananchi kuikosoa serikali na sasa Jeshi la Polisi limejiingiza katika kuisaidia serikali kutimiza matakwa yake ya ukandamizaji wa Demokrasia unaofanywa ndani na nje ya Bunge.
Hivi karibuni vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo vimetangaza kuzunguka nchi nzima kupinga ukandamizaji wa Demokrasia huku cha Mapinduzi (CCM) nacho kikijibu mapigo kuwa kitapita katika sehemu zote ambazo vyama vya Upinzani vitafanya mikutano.