Tarehe June 10, 2016
Hatimaye baada ya bajeti ya Tanzania kwa mwaka 2016/2017 ikiwa imesomwa na kuanza kujadiliwa Bungeni wadau mbalimbali wameanza kutoa maoni kuhusu bajeti hiyo ambapo wanaharakati mbalimbali wakiongozwa na mtandao wa jinsia TGNP wamejitokeza na kupinga vikali bajeti hiyo kwa kile wanachodai kuwa bajeti hiyo imelenga Zaidi kwa sekta binafsi na wafanyabiashara na kuwasahau wananchi wa kawaida ambao ni wazalishaji wakubwa na walipa kodi wakubwa.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Vituo vya taarifa na maarifa Taifa ambaye pia ni Mwenyekiti maarifa wa kata ya makumbusho Bi Janeth Mawiza amesema kuwa vipaumbele ambavyo vimewekwa kwa bajeti ya mwaka huu ni wazi kuwa havimlengi mtu wa pembezoni na badala yake vinawalenga wawekezaji wakubwa na kuwaacha masikini pembeni ambapo ameeleza kuwa kutokana na hali hiyo haitamuwezesha mtanzania masikini kuwa na maisha bora.
Mambo mengine ambayo wanaharakati hao wanadai ni pamoja na kuwepo mfumo shirikishi na endelevu katika kutengeneza na kufutilia utekelezaji wa bajeti.
Kuongezwa kwa bajeti ya maji na afya ambazo wamedai ni ndogo sana na haziwezi kutimiza malengo mazuri hasa kwa wanawake wa Tanzania.