Wednesday, 29 June 2016

‘Tanzania Haitaathirika Uingereza Kujitoa EU’


Tarehe June 29, 2016MELROSEDIANA
Balozi wa nchi Uingereza nchini Tanzania, Dianna Melrose
Siku chache baada ya Uingereza kuamua kujitoa katika Umoja wa Ulaya (EU), Balozi wa nchi hiyo nchini, Dianna Melrose amesema wataendelea kuimarisha uhusiano na Tanzania ili kuhakikisha uwekezaji haupungui.
Akijibu swali kuhusu athari zozote zitakazojitokeza kwa Tanzania baada ya Uingereza kujitoa EU, Balozi huyo alisema kuwa suala hilo haitapunguza uwekezaji, misaada wala vita dhidi ya rushwa na uhalifu wa kimtandao.
“Uhusiano wetu utaendelea kuwa imara kama ulivyokuwa awali,” alisema Melrose.
Tangu Juni 23 Uingereza ilipopiga kura ya maoni kujitoa EU, umetokea mtikisiko mkubwa kati ya Uingereza na washirika wake Wales, Scotland na Ireland Kaskazini, huku hali hiyo ikihofiwa kuweza kuathiri nchi ambazo zina wawekezaji kutoka Uingereza.
Balozi Melrose alisisitiza kuwa Uingereza itaendelea kuwa mwanachama katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (Nato), Umoja wa nchi saba zilizoendelea zaidi duniani (G7), umoja wa mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu kutoka nchi zenye uchumi mkubwa duniani (G20) na Jumuiya ya Madola na kushirikiana na Tanzania.

clouds stream