Tarehe June 19, 2016
Aliyekuwa Mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa Edward Lowassa amesema kuwa Wananchi wanatakiwa kupigania Tume huru ya Uchaguzi kufuatia kutoridhika na matokeo ya Uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka.
Akizungumza kwenye maafali ya Vijana wa Chadema Vyuo vikuu yaliyofanyika katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam leo Lowassa amesema kuwa ili uchaguzi uwe huru na wa Haki ni lazima watanzania wapiganie Tume huru ya Uchaguzi kwa madai kwamba Tume ya sasa ya Uchaguzi ni kama kitengo cha CCM.
Lowassa alisema watanzania wanapaswa kuchukua mfano wa Kenya ambapo wananchi wake wanapigania kuwa na Tume huru ya Uchaguzi ili Uchaguzi uwe wa haki.
Aliongeza kuwa ni lazima Tume ya Uchaguzi yenye mafungamano na CCM iondoke kwa kuwa imeshindwa kumtangaza mtu aliyeshinda uchaguzi na kusisitiza kuwa kamwe hawezi kukubali matokeo ya uchaguzi wa mwaka hata kama ikibidi kufa.
Kwa upande wa ‘Bunge Live’ Lowassa alisema kuwa Bunge kutokuwa Live ni aibu kwa watawala suala ambalo limepelekea heshima yao kushuka na kupitiliza kwa kuwa kila mwananchi ana uhuru wa kuapata Habari.
Katika Uchaguzi mkuu wa Mwaka 2015 Lowassa alikuwa mshindi wa pili kwa kupata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 nyuma ya Rais Magufuli aliyeshinda kwa kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46.