Mazishi ya watu sita walioteketea kwa Moto yafanyika Dar es salaam
Mazishi ya watu sita ambao ni ndugu waliofariki dunia kwa ajali ya moto nyumbani kwao Kipunguni, Manispaa ya Ilala usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita yamefanyika jijini Dares salaam.
Aidha Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal jana aliwaongoza mamia ya wananchi katika mazishi hayo ambayo yamefanyika katika makaburi ya Airwing yaliyopo Ukonga Banana na ibada ya maziko iliongozwa na Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa akisaidiwa na mapadri watano.
Aidha, mara baada ya kuwasili kwa miili yao, Makamu wa Rais aliongoza kutoa heshima kwa marehemu hao kwa kuangalia picha zao, akifuatiwa na Askofu Nzigirwa, Mawaziri Profesa Mark Mwandosya na Dk Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri Dk Milton Makongoro Mahanga, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, wanafamilia na baadaye waumini wachache waliowakilisha umati wa wananchi waliohudhuria.
Katika ibada hiyo, Askofu Nzigirwa alitoa salamu kutoka Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kusema msiba huo ulikuwa mzito, kutokana na kuondoa familia yote kwa wakati mmoja, huku akisema majibu ya maswali waliyonayo watu wengi yapo kwa Mungu.
Naye Makamu wa Rais, akizungumza katika maziko hayo, alisema msiba huo ni mkubwa na aliwapa pole wafiwa na kuwaomba kuwa na moyo wa subira huku akiwaombea marehemu miili yao ilale mahali pema peponi.