Urais 2015: CCM kutegua kitendawili cha makada sita waliofungiwa
Chama cha Mpinduzi (CCM) kupitia kamati kuu ya chama cha mapinduzi (CC), kinarajia kutoa majibu ya makada sita waliofungiwa kutokana na kuanza kampeni za kugombea urais kabla ya muda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Itikadi na unezi CCM Nape Nnauye imesema kwamba Mwenyekiti wa Chama cha Mapinnduzi Dk. Jakaya Kikwete anatarajiwa kuongoza kikao kamati kuu ya Chama hicho Februari 28,2015 jijini Dar es salaam. Katika taarifa hiyo haijafafanua kama kuna ajenda zitakazo zungumzwa katika kikao hicho.
Aidha, kwa mujibu wa chanzo chetu kimoja kutoka ndani ya Chama hicho kimeaimbia Hivisasa kuwa katika kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM, Philip Mangula, atawasilisha ripoti yake ya tathmini dhidi ya makada sita kuona kama walitekeleza adhabu waliyopewa.
Makada ambao waliangukiwa na adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja ni pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye. Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Makada hao walitakiwa kutojihusisha na harakati zozote zinazoashiria kampeni ya kushawishi kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho.
Kutokana na kikao hicho inawezekana kuwa wapo watakaotangazwa kuwa huru. Hata hivyo kwa wale ambao bado walikuwa wakiendelea na harakati za kufanya kampeni ya kushawishi kinyume cha utaratibu wanaweza kupoteza sifa za kuwania urais mwaka huu.