UN yailaumu Tanzania kuruhusu FDLR kufanya mikutano
Taarifa hiyo ya Umoja wa mataifa inasema kuwa tangu mwaka wa 2013, viongozi wa FDLR na baadhi ya washirika wao wa kisiasa kutoka Ulaya wamekuwa wakikutana nchini Tanzania.
Lakini wachunguzi wa Umoja wa mataifa walipoiuliza serikali ya Tanzania kujibu madai haya ilikanusha kabisa kuwahi kukaribisha mikutano yoyote ya waasi ndani ya ardhi yake na kuongeza kuwa hakujawahi kuwa na mazungumzo yoyote kati ya majeshi yake na wapiganaji wa FDLR.
Umoja wamataifa umesema pia kuwa kuna ushahidi wa pesa zilizotumwa kutoka taifa hilo la Afrika Mashariki kwa baadhi ya washukiwa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Kundi la FDLR, liliundwa mwaka wa 2000 na wahutu waliokimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia mauaji ya kimbari ya Rwanda. Kundi hilo linapinga utawala wa kitutsi na ushawishi wake katika eneo la maziwa makuu.