Wahitimu JKT kufanya maandamano siku 3 jijini Dar es salaam
Wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wametangaza kufanya maandamano ya siku tatu mfululizo usiku na mchana jijini Dar es Salaam kuanzia Jumatatu ijayo. Maandamano hayo yanatarajiwa kushinikiza kuonana na Rais Jakaya Kikwete kumweleza matatizo ya ajira wanayokabiliana nayo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Vijana waliohitimu mafunzo ya JKT, George Mgoba alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakiomba kukutana na Rais ili wamueleze matatizo yao bila mafanikio huku wakipewa ahadi za uongo na Katibu Mkuu wa Rais.
Ameongeza kuwa wameandika barua nyingine na hivi karibuni Katibu wa Rais aliwapigia simu kuwa wafike Februari 10 ili waonane na Rais na walipofika, hawakufanikiwa kumuona Katibu huyo.
Amesisitiza kuwa sababu za kutaka kuonana na Rais ni kutaka kujua hatma yao ya kutopatiwa ajira kutokana na mafunzo ya kijeshi waliyoyapata ambapo hivi sasa wao ni askari kamili.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti, Paral Kiwango, amesema suala la wao kuapata ajira linaonekana kuwa na upendeleo mkubwa, kwani wenzao wa upande wa Zanzibar wote waliomaliza mafunzo ya JKT, wamepata ajira wanashangaa kwa upande wa Bara wao wakiendelea kusota tu uraiani hadi hivi sasa.
Mtandao wa Hivisasa unaendelea kumtafuta Kamanda wa Kanda maalumu ya Dar es salaam Suleiman Kova atolee ufafanuzi dhidi ya maandamano hayo.