Uwanja wa sasa wa Stamford Bridge

Klabu ya Chelsea ya Uingereza imepewa idhini na baraza la wilaya kujenga uwanja mpya mradi ambao utagharimu £500m.
Uwanja huo utakuwa na uwezo wa kutoshea mashabiki 60,000.
Kamati ya mpangilio wa wilaya ya Hammersmith na Fulham imeidhinisha mpango wa kubomoa uwanja wa sasa wa Stamford Bridge unaotoshea mashabiki 41,000.
Miongoni mwa yaliyomo kwenye mpango mpya wa ujenzi, ni pamoja na kujengwa kwa njia ya kutumiwa na watu kutembea kutoka kituo cha reli kilicho karibu.
"Tunashukuru kwamba mpango wetu umeidhinishwa," Chelsea walisema kupitia taarifa.
"Uamuzi wa kamati hiyo hata hivyo hauna maana kwamba tunaweza kuanza ujenzi mara moja. Hii ni hatua tu ya karibuni zaidi, ingawa ni hatua muhimu sana, ambayo ilikuwa ni lazima tuitimize kabla ya kazi ya ujenzi kuanza, pamoja na kupokea vibali vingine."
Meya wa London Sadiq Khan atakuwa na usemi wa mwisho kuhusu ujenzi wa uwanja huo mpya.
Ramani ya uwanja huo mpya imechorwa na wasanifu mijengo Herzog na de Meuron, ambao pia walichora uwanja wa Olimpiki wa "Birds Nest" mjini Beijing.

Hatua ya kutolewa kwa idhini ya kujengwa kwa uwanja huo inamaanisha kwamba sasa huenda Roman Abramovich akatafuta uwanja wa muda wa kutumiwa na viongozi hao wa sasa wa Ligi ya Premia kwa karibu miaka mitatu ujenzi utakapokuwa ukiendelea.
Viwanja ambavyo wanaweza kutumia ni Twickenham na Wembley.
Chelsea huenda hata hivyo wakatatizika kuupata uwanja wa Wembley kwani utatumiwa na wapinzani wao Tottenham Hotspur angalau kwa msimu wa 2017-18 wanapomalizia ujenzi wa uwanja wao wa kutoshea mashabiki 61,000.
Chelsea wanaweza bado kuendelea kutumia Stamford Bridge ujenzi ukiendelea, lakini mpango huo utakuwa ghali.
